WANAWAKE MWANZA WAJA NA SACCOS MOJA KUWAUNGANISHA MAKUNDI YOTE
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewapongeza wanawake mkoani humo kwa kuazisha SACCOS itakayowaunganisha kwenye sekta ndogo ya fedha na kuhakikisha wanakua kitu kimoja kwa kuwaunganisha makundi yote ndani ya mkoa huo.
Mhe. Mtanda ametoa pongezi hizo leo Novemba 06, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa semina ya uhamasishaji wa kuanzisha SACCOS ya wanawake Mkoani humo iliyofanyika katika ukumbi wa Nyanza Coperative Union.
Aidha, amewataka wanawake hao kuitumia vizuri Ofisi ya Mrajisi Msaidizi na CRDB foundation kupitia programu ya IMBEJIMU kupata elimu ya fedha, umuhimu wa kuhifadhi sehemu salama, elimu ya biashara na ikasaidie kuwapa elimu akina mama wengine ili waweze kukuza mitaji.
"Sekta ya fedha inajumuisha taasisi zote zinazojihusisha na huduma ya fedha zikiwemo microfinance ambapo kwa sehemu kubwa ni SACCOS, hii imedhihirisha ukweli kwamba sekta hii inayogusa vikundi vya wananchi wa hali ya kati na chini imekua na mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi." Mtanda.
Akisisitiza umuhimu wa SACCOS, Mhe. Mtanda amesema mwaka 2024 Mwanza imesajili SACCOS hai 41 kwenye mfumo wa kielekitroniki na kupatiwa leseni za biashara zenye wanachama 14, 000 wenye hisa na wana amana za bilioni 27.7 na kwamba mikopo iliyotolewa kwa wanachama hao ni Bilioni 2.4.
Hilda Boniface, Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Mwanza amesema lengo la kuanzisha chama hicho ni kuunganisha vyama mbalimbali ndani ya Mkoa wa Mwanza na kuwa na chama kikubwa na imara kama vyama vya mazao zaidi ya 200, vyama 24 vya wavuvi, akiba na mikopo 41.
Vilevile, amesema kupitia umoja huo wanawake watahamasisha uzalishaji kwenye zao la pamba ambalo kwa sasa limekua likisuasua, kukomesha kabisa wizi wa samaki kwenye vizimba vya kisasa vya wavuvi pamoja na kukomesha tabia ya kutorejesha mikopo kwa wanachama kwenye vyama vya akiba na mikopo.
Aidha, amefafanua kuwa kupitia umoja huo itakua fursa sasa kwa makundi mbalimbali ya kitaaluma kujiunga kwa kujisajili kama fungamani za pamoja na kuhakikisha kunakua na chombo kimoja imara kiuchumi ndani ya mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.