Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mkoa wa Mwanza wametakiwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa umakini, ubora na viwango ili iwe yenye tija kwa wananchi na idumu kwa muda mrefu.
Rai hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bi. Salome Mwakigomba katika kikao cha Wataalam cha Tathmini ya utekelezaji wa kipindi cha pili cha Mpango wa TASAF Mkoa wa Mwanza.
Bi. Mwakigomba amewataka Waratibu hao kusimamia miradi hiyo iwe endelevu na ikamilike kwa wakati, ambapo amesema wao nia yao ni kuiunga mkono Serikali kwa kuibua na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo pia ni lazima ijengwe kwa ufanisi ili idumu.
“Ni mtarajio na matamanio yetu kwamba miradi yetu hii ya TASAF itekelezwe kwa ubora, kwa mfano mimi nimesoma shule ya Jitegemee imedumu kwa muda mrefu bila kuharibika hivyo natamani hata miradi yetu idumu pia kwa kipindi kirefu”.
Kazi ya TASAF ni ibada unamsaidia mtu kula na kujikimu, hukumu ya mwisho inasema nilikuwa na njaa ukanipa chakula, kwa sasa Mtu anaweza kujitafutia na akapata kitu hiyo ni ibada. Tusichukulie kazi kama kazi tuchukulie matokeo ya kazi na wangapi watanufauka katika ubora ule ule. Amesema Bi. Mwakigomba.
Aidha ametoa muda wa mwezi mmoja hadi kufikia septemba 10, miradi yote ya TASAF katika Mkoa wa Mwanza iwe imekamilika na kukabidhiwa kwa kuwa hakuna kikwazo chochote cha rasilimali hivyo hakutakuwa na sababu yoyote ya kushindwa kufanya hivyo.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa, Mhandisi Chagu Ng’oma Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu ametoa wito kwa Waratibu hao wa TASAF kushirikiana kwa ukamilifu na Wahandisi wa Wilaya katika miradi ya ujenzi ili kuwepo na ubora, viwango katika utekelezaji wa miradi.
Amesisitiza kuwa uwepo wa wazo na ushauri kutoka kwa Wahandisi kwa pamoja na waratibu mashauriano hayo ni bora na yanaweza kuleta mchango chanya katika utekelezaji ili kupatikana kwa miradi bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.