Wataalamu wa Afya Mkoani Mwanza wametakiwa kutoa elimu ya chanjo zinazotolewa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya ili kuongeza hamasa kwa wananchi kupeleka watoto.
Agizo hilo limetolewa mkoani hapa na Mkuu wa Mkoa, Mhe. John Mongella wakati wa akizindua chanjo ya rubella na surua kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Alisema Wataalamu wote wa Afya waliopata mafunzo ya utoaji chanjo hiyo lazima pia wahakikishe wanatumia muda wao kutoa elimu ili kwa wale ambao bado hawana ufahamu wahamasike kupeleka watoto wao kupatiwa chanjo.
"Leo tupo hapa kuzindua rasmi zoezi la utoaji chanjo hii mkoani kwetu huku lengo letu kwa mwaka huu ni kuhakikisha tunafanikiwa kwa asilimia mia moja."
"Sote tunafahamu kuna wakati zoezi linashindwa kufanikiwa kwa kwa sababu kuna baadhi ya wananchi wetu bado hawana uelewa na wana mila potofu juu ya chanjo hii basi ni jukumu lenu wataalamu wa afya kuhakikisha mnatoa elimu kwa watu wote ili kuwaongezea chachu ya wao kuleta watoto wao kuchanjwa.
"Kwani mpaka sasa Maandalizi yameshakamilika na chanjo itaanza kutolewa leo hivyo ni wajibu wa kila Kiongozi toka ngazi ya mtaa hadi wilaya kuhakikisha anasimamia zoezi hili ili lisije likaingia dosari kwa kuwa uwekezaji ni mkubwa sana.
"Mwisho niwakumbushe wananchi wote kama kauli mbiu inavyosema "Chanjo ni kinga kwa pamoja tuwakinge" kwa hiyo wote wazazi na wasio wazazi tuwajibike na tuifanyie kazi kauli mbiu hii ili tufikie malengo kama mkoa na Taifa kwa ujumla.
Awali akitoa taarifa fupi ya chanjo hiyo mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt.Thomas Lutachunzibwa aliwataka wananchi kupeleka watoto kwa wingi kupata chanjo kwani imethibitishwa na shirika la Afya duniani WHO.
"Kwa mwaka huu matarajio ya mkoa ni kuwafikia jumla ya watoto zaidi ya laki tisa katika vituo 608 vilivyoandaliwa ambapo kwa chanjo ya rubella na surua lengo ni watoto 667 579 na polio ni watoto 266 140.
"Mara ya mwisho chanjo hii ilitolewa mwaka 2014 ambapo ufanisi ulikuwa ni asilimia 97 hivyo niwaombe wanaanchi kwa mwaka huu tuwapeleke watoto kwa wingu wapatiwe chanjo ili ufanisi iwe mkubwa zaidi," alisema Dkt.Lutachunzibwa.
Kwa upande wake Katibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Dkt. Zainabu Chaula amewataka wakazi wa Mwanza na Tanzania kuhakikisha wanaunga mkono chanjo hiyo.
"Chanjo hii ni moja ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa inafikia maadhimio ya kutokomeza kabisa magonjwa yasiyokuwa yakuambukizwa kwa watoto wadogo.
"Niwaombe wote kwa pamoja tuwapeleke watoto wetu wakapate chanjo kwani Serikali yetu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya uwekezaji mkubwa ili kufikia malengo ya Afya bora kitaifa,"alisema Dkt. Chaula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.