Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amewataka watanzania wasifurahie kuzaa bali wanapaswa kutambua kulea na kumtunza mtoto katika maadili mema ni jukumu la wazazi na si vinginevyo.
Kauli hiyo aliitoa jijini Mwaza katika ziara yake ya kuendelea kutembelea magereza mbalimbali na kuzungumza na wafungwa na mahabusu ambapo alisema ameshuhudia watoto chini ya miaka 18 akiwa katika magereza lakini wengi wao wakiwa na kesi ndogo ndogo.
“Jamani tukumbuke watanzania tunakadiriwa kufikia milioni 55, kwa hiyo msongamano wa watu magerezani unatokana na ongezeko la watu lakini jambo ambalo nimeliona kule hasa kwa upande wa watoto, wengi wao wapo kule kutokana na kukosa malezi mazuri na msaada kutoka kwenye familia zao.
Mganga ambaye jana alikuwa katika Wilaya ya Sengerema na Ukerewe, aliwataka mahakimu na polisi kuangalia kesi ambazo zinaweza kumalizwa kwa mazungumzo ya kuwashauri au kuwapa adhabu mbadala bila kuwapeleka magarezani.
Kwa upande wa Waziri wa Katiba na Sheria,Mhe. Balozi Dkt. Agustino Mahiga alisema baada ya ziara hiyo ya kutembelea mikoa yote atakwenda kuzifanyia kazi changamoto zote atakazokutana nazo zikiwamo upungufu wa mahakama ambapo aliahidi kwamba lengo la Serikali ni kuona kila wilaya inakuwa na mahakama ya mwanzo naya wilaya.
“Kama mnakumbuka Mhe.Rais Dkt. John Magufuli alifanya mabadiliko na mimi nikaletwa katika wizara hii hivyo bado ni mgeni, ziara hii inakuwa na mambo mengi likiwamo kujitambulisha na kuona kwa uhalisia changamoto zilizopo ambazo hata wabunge wamekuwa wakizisema bungeni.
“Jambo ambalo mpaka sasa nimeliona ni ratio (kiwango) cha watu waliopo magerezani ni kukibwa kuliko uwezo wake, yaani kila palipo na mfungwa mmoja kuna mahabusu wanne, sasa kwanza nitaanza kuhakikisha mahakama za mwanzo na wilaya zinajengwa, pia tutaangalia idadi ya watumishi,”alisema.
DPP Mganga aliwachia huru wafungwa na mahabusu 325 katika magereza mbalimbali Kanda ya Ziwa wakiwamo askari nane wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakituhumiwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 1/2019 ya dhahabu yenye uzito wa kilo 323.6 na fedha taslimu Sh. milioni 305.
Katika gereza la Butimba jijini Mwanza aliwaachia huru wafungwa na mahabusu 75, Shinyanga 25, Kahama 43, Mugumu 52, Bunda 24, Bariadi 100 na Tarime 6.
Alisema sababu zilizofanya kuachiliwa kwa mahabusu na wafungwa hao ni kubambikiwa kesi, ugonjwa, umri na tuhuma nyingine zenye harufu ya rushwa kuanzia kwa raia wenyewe kwa wenyewe, mpelelezi hadi kwa hakimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.