Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amewasihi Watanzania kuuenzi muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kutobaguana na kuuchukulia Muungano kama nguzo ya mafanikio na kufanya kazi kwa bidii
Mhe. Malima amesema hayo leo Aprili 26 2023 katika Maadhimisho ya Miaka 59 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo ki mkoa yamefanyika katika wilaya ya Kwimba na kuongoza uzinduzi wa zoezi la upandaji miti kwenye Chuo cha ufundi Veta ambapo Mkoa wa Mwanza umejipanga kupanda miti milioni 23
"Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta mambo mengi ya kimaendeleo na waasisi wetu walituasa Muungano uende pamoja na kufanya kazi ili kulijenga Taifa letu," Amesema Mhe. Malima
Mbali ya zoezi hilo la upandaji miti,Mhe. Malima katika kutekeleza azma ya Muungano ni kazi ya kuijenga nchi,amezindua mradi wa maji kwenye Kijiji cha Malembe kata ya Igongwa Wilayani Kwimba iliyogharimu zaidi ya Shs milioni 900 na kuwataka wananchi kuilinda miradi hiyo kwa faida ya vizazi vijavyo.
" Naishukuru Serikali hii ya awamu ya sita imeonesha kutujali wananchi wa Mwanza kwa kutupatia miradi ya kimkakati ambayo inachochea maendeleo katika mkoa wetu,". Amesema Mkuu huyo wa Mkoa
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija amesema wanajivunia na kuishukuru serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea fedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kijamii
" Wananchi wa Kwimba na maeneo ya jirani tunaishukuru na tunajivunia miundombinu na uwekezaji mkubwa ambao Rais wetu ameufanya kwenye Wilaya yetu ya Kwimba kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kijamii,". Amesema Mhe. Ludigija
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa ametumia maadhimisho hayo kuwaelimisha wazazi juu ya umuhimu wa chanjo na kuwahamasisha kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata huduma hiyo.
" Nitoe rai kwa wazazi kuhakikisha watoto wote wanaostahili kupata chanjo wanapelekwa katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuhakikisha wanajikinga na magonjwa,". Amesema Dkt. Rutachunzibwa
Tanzania huadhimisha Sherehe za Muungano kila ifikapo Aprili 26 huku Watanzania wakifanya shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa kama ishara ya kuuenzi Muungano huo uliofanywa na waasisi wetu Mwl Julius Nyerere na Abeid Karume Aprili 26,1964.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.