Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii , Polisi ,Raiway Children Africa ,WoteSawa na mashirika yasiyo ya serikali wametakiwa kushirikiana na serikali kutoa elimu ya haki za watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani na wafanyakazi wa nyumbani.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmily Kasagala wakati wa utambulisho wa mradi mpya wa kuwezesha upatikanaji wa haki za wafanyakazi wa nyumbani na watoto na vijana wanaoishi na kufanyakazi mitaani kupitia kutoa elimu ya sheria katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana.
Alisema ushirikiano huo utasaidia kutatua matatizo ya watoto wa makundi hayo na kuzuia ongezeko la kuja mitaani na kupunguza unyanyasaji wa wafanyakazi wa majumbani hivyo kila mmoja aone anao wajibu wa kumlea na kumwongoza mtoto ili afikie malengo yake ya badaye.
Alisema suala la watoto wadogo kushinda mitaani , unyanyasaji wa wafanyakazi wa nyumbani ,usafirishaji haramu wa watoto siyo sahihi kutokana na haki wanazostahili kupata kwa kujibu wa sheria ya mtoto hivyo wakati umefika wa kukabiliana na sababu zinazochangia watoto kukaa mitaani,kunyanyaswa na usafirishaji haramu .
Alisema ndani ya mwaka mmoja Railway Children Africa na Wotesawa wamewaokoa watoto 353, ambapo wamewarejesha nyumbani watoto wapatao 193 na wamefanikiwa kutoa msaada wa kisheria kwa watu 274 na kutoa mafunzo na kuwawezesha kiuchumi familia na vijana 189 huku wakiwaunganisha shule na mafunzo mbalimbali ya ufundi watoto 316.
" Tunatambua zipo sababu nyingi zinachangia adha hii ni vitendo vya ukatili ngazi za familia,vitendo vya ukatili mashuleni,ugomvi miongoni mwa wazazi au walezi,kuachana kwa wazazi,hali duni ya uchumi wa familia ,waajiri wa wafanyakazi kutokuwa waadilifu, ukosefu wa elimu ya sheria ya mtoto,kutofanya Kazi kwa kamati za ulinzi wa mtoto ngazi ya kata na vijiji na changamoto za makundi rika naimani na huu mradi mpya utaleta nuru " alieleza Kasagala
Alisema serikali inatambua juhudi zinazofanywa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika kuchangia katika mpango wa taifa wa ulinzi wa watoto kwa mwaka 2017/ 2018 na 2021 hadi 2022 japokuwa takwimu za watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na wanaofanya kazi za nyumbani katika Mkoa wa Mwanza zinaonekana kukua na kuongezeka kadri siku zinavyokwenda .
Alisema kutokana na zilizopatikana hivi karibuni kutokana na zoezi lililoendeshwa kati ya shirika Railway Children Africa kwa kushirikiana na PACT Tanzania na Cheka sana Tanzania pamoja na serikali kupitia Halmashauri za Ilemela na Jiji la Mwanza zinaonyesha kuna watoto 1254 waliohesabiwa mitaani ambapo watoto 978 (78%) , waliohesabiwa nyakati za mchana na 276 (22%) nyakati za usiku.
Aliongeza kuwa kupitia utafiti uliofanyika mwaka 2020 wa kumlinda mtoto nchini kwa kutathmini kuongeza wigo na matokeo ya matumizi ya sheria ndogo zinazomlinda mfanyakazi wa nyumbani unaonyesha manispaa ya Ilemela na Nyamagana kuna wafanyakazi wa nyumbani 6,286 .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la WoteSawa ambaye pia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Raiway Children Africa Angela Binedcto alisema wanatamani kuona jamii ambayo ni salama ,huru na uwazi pamoja na uwepo wa mfumo wa sheria ambayo itaonyesha wafanyakazi wa nyumbani wanafanya kazi katika mazingira salama.
Alisema watoto hao wanakabiliana na matatizo mengi ikiwemo ukatili wa kingono na malipo yasiyoendana na utendaji Kazi wao hivyo kupitia mradi huo WoteSawa na Raiway Children Africa wataimarisha kukuza mifumo ya utoaji haki na msaada wa kisheria kwa wafanyakazi wa nyumbani , watoto na vijana wanaoishi na kufunya Kazi mtaani.
Aliongeza kuwa wataongeza kuelewa na ujuzi kwa jamii kuhusu ulinzi wa haki za watoto huku matarajio yao yakiwa ni kuongezeka upatikanaji wa msaada wa kisheria na saikolojia kwa makundi hayo pia mradi huo utafanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kirumba, Buhongwa,Igoma,Kayenze,Luchelele,Kitangiri , Bugarika ,Mkuyuni Buswelu ,Machina,Igogo , Mabatini na Bugongwa.
Naye Kaimu Meneja wa Shirika la Railway Children Africa Mkoa wa Mwanza Mary Mushi alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja 2020 wameweza kuoka kutoka mtaani watoto wapya 291,walitoa huduma za afya kwa watoto 240, huduma ya chakula kwa familia 91,kusaidiwa kuanganishwa na shule na kupewa vifaa watoto 301,kuwapeleka vijana 83 katika vyuo vya elimu ya ufundi, ,waliowezesha vijana 57 kufanya ujasiliamali,waliwaunganisha na kuwarejesha watoto143 na familia zao huku familia 72 ziliwezeshwa kibiashara.
Alisema mradi huo mpya utawapa wigo na kufanya kazi na jamii zaidi na kuleta chachu itakayosaidia kuondokana matatizo hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.