Watumishi wa Afya ongezeni bidii katika kuwahudumia wananchi: RAS Mwanza
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amefanya ziara ya kikazi kwenye Kituo cha Afya Igoma kwa lengo la kuwasikiliza watumishi na kupata maoni yao kuhusu kuboresha utendaji kazi na mazingira ya kufanyiakazi.
Akizungumza na watumishi hao Alhamisi hii, Ndugu Balandya amesema kada ya afya ni nyeti ambayo inagusa uhai wa mwanadamu hivyo watumishi hao ni lazima watangulize viapo vyao kwa kufanya kazi kwa weledi.
"Leo nimefika hapa mahsusi kwa ajili ya kuja kuwasikiliza ninyi na ndio maana sikuwa na hotuba," alisema Balandya. Nimewasikia changamoto zinazowakabili ambazo nyingi ni za kuboresha mazingira yenu ya kazi, nawaahidi zitafanyiwa kazi haraka na Mkurugenzi wa Jiji atalisimamia hilo na kunipa taarifa pia maafisa utumishi shughulikieni changamoto za Watumishi kwani nyingi siyo tatizo tena zipo ndani ya uwezo wenu," amefafanua Mtendaji huyo.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Bi.Claudia Kaluli amewataka watumishi hao kubadilika na kufanya kazi kwa bidii kutokana na tathmini iliyofanywa kuonesha utendaji wa kazi usioridhisha kwa kituo hicho cha Afya.
"Niwaombe sana watumishi wenzangu,tangulizeni uzalendo haya malalamiko ya wananchi hayaleti sura nzuri kwa kada yetu ya afya,"Kaluli
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili watumishi hao wa kituo cha afya Igoma ni pamoja na kuchelewa kupanda vyeo, kubadilishiwa kada, kuchelewa kulipwa stahiki za likizo na uhamisho, kukosekana kwa umeme wa uhakika japo Kangavuke ipo pamoja na kuongezewa eneo la kituo hicho na kuboreshewa barabara ya kuingia kituoni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.