Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza Joachim Otaru, ametoa rai kwa watumishi wa Afya wanaojitolea kujituma ili kusaidia juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya kwenye maeneo watakayonufaika na mradi wa kuwalipa nusu ya mshahara wa ajira rasmi.
Ametoa wito huo mapema leo Agosti 15 2022 wakati akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza kwenye hafla ya Uzinduzi wa mpango wa kujitolea kwa watumishi wa huduma za afya unaoratibiwa na Taasisi ya Mkapa kwa kushirikiana na Serikali utakaowanufaisha watumishi 152 Mwanza na Simiyu.
Vilevile, ndugu Otaru amezipongeza Wizara za TAMISEMl na Afya kwa kupandisha hadhi vituo vya kutolea huduma kutoka Zahanati kuwa Vituo vya Afya au Hospitali za Wilaya na wadau mbalimbali wanaoshiriki juhudi za Serikali za kuboresha huduma za Afya huku akibainisha kuwa mradi huo utasaidia kukuza ujuzi na uzoefu kwa wataalamu hao wakati wakisubiri ajira rasmi.
"Nawapongeza taasisi hii kwa kuamua kutusaidia kupunguza tatizo la upungufu wa wahudumu kwenye sekta ya afya, pia natoa wito kwa mchakato wa kuwapata watoa huduma hizi uzingatie miongozo na taratibu za kiutumishi kwa kupata sifa stahiki nasi tupo tayari kushirikiana nao." Amesema, Katibu Tawala Msaidizi, Utumishi na Rasilimaliwatu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza, Daniel Machunda.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Deogratius Kayombo ameishukuru taasisi hiyo kwa kuona tatizo na kuchukua hatua kushirikiana na Serikali kwenye kutatua ama kupunguza Upungufu wa watoa huduma za afya ambao kwa kuanzia mradi huo unatekelezwa kwenye mikoa ya Mwanza, Simiyu, Lindi na Mtwara.
Dkt. Ellen Senkoro kutoka Mfuko wa Benjamin Mkapa amesema kutokana na tatizo la upungufu wa 50% ya watumishi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, taasisi hiyo iliandaa muongozo wa kujitolea kwa Watumishi wa Idara ya Afya ambao ulizinduliwa Septemba 2021 na Waziri wa Afya ukilenga.
Aidha, Dkt Senkoro amefafanua kuwa mpango huo utasaidia kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, Kupambana na maambukizi ya UKIMWI/VVU, huduma za Chanjo ya Uviko 19 na zingin na kwamba taasisi hiyo imeshaajiri watumishi 4159 na Asilimia 50 wamehuishwa kwenye ajira rasmi za Serikali kadiri vibali vya ajira ya afya vinapotolewa na serikali.
Warsha hiyo imewashirikisha Waganga wakuu wa Halmashauri, Maafisa Utumishi wa Mikoa, Makatibu wa Afya, Mashirika yasiyo ya serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wizara ya Afya na wizara ya TAMISEMl.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.