WATUMISHI WAKUMBUSHWA KUFANYA MAZOEZI KUEPUKA MAGONJWA
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Mhandisi Chagu Ngh'oma ametoa wito kwa watumishi wa umma Mkoani humo pamoja na wananchi kwa ujumla kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza na kujenga nguvu kazi yenye afya bora.
Ametoa wito huo leo Januari 18, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa katika hotuba aliyoitoa baada ya Matembezi ya Kilomita tano yaliyolenga kuwakusanya pamoja watumishi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa na ofisi zingine kwenye mazoezi ya kuimarisha afya.
"Ofisi ya mkuu wa mkoa kwa kutambua umuhimu wa afya kwa watumishi wake imeweka utaratibu wa mazoezi mara baada ya saa za kazi mara 3 kwa wiki jumatatu, jumatano na ijumaaa na kila Jumamosi ya tatu ya mwezi hivyo nawasihi tuzingatie utaratibu huu kwa faida ya afya zetu," amesisitiza Ngh'oma.
Ameongeza kuwa licha ya mazoezi jamii inapaswa kuepuka vyakula vya wanga na mafuta na badala yake kula mbogamboga, matunda na maji mengi kwani magonjwa yasiyoambukiza yanachangiwa na mtindo wa maisha.
Aidha, ametoa wito pia kwa watumishi wote wa Sekretarieti ya Mkoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na tatasisi zingine za kuhakikisha wanashiriki kikamilifu mazoezi hayo kwa afya bora.
Katika matembezi ya leo ya kilomita 5 watumishi walipita baadhi ya mitaa mbalimbali iliyopo katikati ya Jiji la Mwanza na pia walipata fursa ya kupimwa afya zao hususani magonjwa yasiyoambukiza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.