Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amemuagiza Katibu Tawala Mkoa huo kuwasimamisha kazi kwa Siku Saba Mkuu wa Idara ya Ardhi Robert Phales, Ayubu Kasuka Halima Nassor na Yuster Zephrine kuanzia leo Januari 13, 2023 ili kupisha uchunguzi kutokana na utovu wa nidhamu.
Mhe. Malima ameongeza kuwa Ofisi yake imeandika Barua TAMISEMl ya kuomba achukuliwe hatua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Ndugu Sekiete Yahya kwa kukiuka Maelekezo ya Kamati ya Usalama Wilaya ya Tarehe 28, 09, 2022 yaliyozuia uuzwaji wa Viwanja Namba 194 na 195 vilivyopo kwenye mtaa wa Rwegasore na wao kuamua kuviuza kwa Milioni 500 kila kimoja.
"Tumemkuta Mkurugenzi wa Jiji na Makosa makubwa sana ya kukiuka maelekezo ya Kamati ya Usalama Wilaya na ameonesha aheshimu kabisa Mamlaka zilizo juu yake kwa utovu huo wa nidhamu alioufanya ambapo alitengeneza hoja ya kuuza viwanja hivyo isivyo halali na tumebaini kuwa endapo vingeuzwa kwa njia ya Mnada basi vingeuzwa kwa zaidi ya Milioni 500 kila kimoja."
Katika hatua ingine, Malima amesema Ofisi yake imeunda Kamati ya kuchunguza Sakata hilo kwa siku Saba itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Maadili wa Kanda ya ziwa Ndugu Godson Kweka huku ikihusisha wataalamu kutoka Ofisi za TAKUKURU, Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa pamoja na Ofisi ya Mashtaka (DPP).
"Terehe 28, 9, 2022 Kamati ya Usalama Wilaya iliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Jiji isiviuze viwanja namba 191 hadi 195 vilivyopo kwenye mtaa wa Rwegoshora bila ya idhini ya Kamati hiyo lakini wao wakaamua kuviuza kwa Tshs Bilioni Moja." Malima amefafanua.
Amefafanua kuwa, awali Kamati ya Usalama Mkoa imefanya uchunguzi na kubaini kuwa viwanja hivyo vimeuzwa kinyemela bila kumtaarifu Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na Halmashauri imekiri kuviuza na kusema wamefanya hivyo kwa ruhusa ya Ofisi ya Rais Ikulu, TAMISEMl na Wizara ya Ardhi jambo ambalo si kweli.
"Viwanja hivi haviruhusiwi kuuzwa, kufanyiwa Ujenzi wala kuendelezwa kwa namna yoyote mpaka pale suala hili litapomalizika na endapo itaonekana wamiliki wanastahili kuendelea watapata taarifa na kwa upande wa Halmashauri nnaagiza fedha zilizopatikana kwenye uuzwaji wa viwanja hivyo zisitumike ili itapobainika kumekua na ukiukwaji wa uuzwaji basi wamiliki watarejeshewa fedha zao." Mhe. Malima.
Katika hatua ingine Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetoa Onyo kali kwa Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Watumishi wa Idara ya Fedha na Uhasibu, Afisa Manunuzi, Mwanasheria na Mkaguzi wa Ndani kujitathmini kwenye Utendaji wao kwani wameonekana kutosaidia Halmashauri ipasavyo na itatoa Onyo kali kupitia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa.
"Mwanza haiwezi kuwa kichwa cha Mwendawazimu kwamba kila mmoja anakuja kupiga pesa, kama watu wameingia kufanya tamaa na kuhusika na suala hili basi kwa dhamira yetu kama Viongozi wa Mkoa tutakwenda kutoa mfano kwenye suala hili kwa kutoa adhabu kali." Mkuu wa Mkoa.
Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa ameiagiza Halmashauri ya Jiji kuboresha Mazingira Rasmi ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) ili wafanye biashara kwa utulivu na kukomesha tabia ya kufanya biashara kiholela kwenye mji huo hali inayochafua taswira ya Mkoa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.