WAZAZI MSIWANYANYAPAE WATOTO WENYE DOWN SYNDROME - RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa jamii kuwajali watoto wenye tatizo la Down Syndrome na kuhakikisha wanawapatia huduma za kijamii kama elimu na afya na kuacha tabia ya kuwatenga na kuwanyanyapaa.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo tarehe 21 Machi, 2025 wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Down Syndrome Kitaifa kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Maadhimisho yaliyofanyika katika viwanja vya Furahisha.
"Watu wenye ulemavu wana uwezo wa kufanya mambo makubwa sana, tusiwafiche watoto wenye tatizo hili wala ulemavu wa aina yoyote, na tuwakumbushe kuwa watakaowalea vizuri wenye tatizo hili basi mbele ya Mwenyezi Mungu wana daraja na fungu lao la thawabu." Mhe. Mtanda amefafanua.
Aidha, ametoa wito kwa watoa huduma za kijamii mathalani sekta ya afya kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa matamko ya Serikali na namna ya kutekeleza katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa kundi hilo kwa mujibu wa sera ya afya inavyotambua kisheria.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amewataka wazazi wanapokuwa wajawazito wafanye hima kufika kwenye vituo vya huduma kwa uchunguzi na kufuata ushauri wa wataalamu na amebainisha kuwa Usonji inasababishwa na Chromosome kuzidi hadi 47 kutoka 46 za kawaida kwa binadamu na kusababisha kuwa na zaidi ya mfumo wa jinsi ya ukuaji wa ubongo na mwili na kwamba wenye hali hiyo wakipata msaada wanaweza kukua kiafya na kuwa na furaha na kuleta tija katika jamii wanayoishi.
Naye, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Down Syndrome nchini Bi. Mony Teri Pettit ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha kunakuwepo na mifumo bora ya kupata huduma za kijamii inaboreshwa hususan elimu na afya kwa kupatiwa huduma hizo na bila malipo na kujumuishwa kwenye stadi mbalimbali.
Bi. Anna Barnabas Mzazi wa mtoto mwenye Down Syndrome amewataka wazazi kuwalea watoto wenye tatizo hilo kwa upendo na ameiomba Serikali kufanya vipimo mara tu mtoto anapozaliwa ili kuwabaini na siyo kubahatisha katika matibabu kama ambavyo mwanaye alikosewa na kumsababishia kushindwa kuzungumza hadi sasa.
Siku ya Kimataifa ya Down Syndromes ambayo kitaifa imefanyika Mwanza imepata heshima ya kuadhimisha imechagizwa na kaulimbiu isemayo ; Mifumo ya Huduma za Kutuwezesha Iboreshwe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.