WAZAZI TIMIZENI WAJIBU WA KUWALEA WATOTO WENU -RC MTANDA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda leo Aprili 14,2025 amezindua rasmi mkakati wa kutokomeza watoto wa mitaani na kutoa rai kwa wazazi kutimiza wajibu wao wa malezi.
Akizungumza na makundi mbalimbali yanayojihusisha na malezi kwa watoto na watoto wa mitaani kwenye ukumbi wa Ofisi yake Mtanda amesema chanzo cha kuwepo kwa watoto mitaani ni wazazi kushindwa kutimiza majukumu yao ya ulinzi na malezi bora kwa watoto wao.
"Nichukue nafasi hii leo kuhimiza hili jambo, ile adhabu ya kulipa Tshs. Milioni 5 au kifungo cha miezi sita jela ipo palepale kwa wale wazazi watakaobainika kwenda kinyume cha sheria nawasihi wadau mliopo hapa tushikamane kutoa elimu kwa jamii",Mkuu wa Mkoa.
Aidha amebainisha migogoro ndani ya familia,umasikini,pamoja na kutoandikwa mirathi nayo imechangia kuwepo kwa ongezeko la watoto wa mitaani.
Ameyapongeza pia mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na watoto wa mitaani kwa kujisajili rasmi na kufanya shughuli zao kwa kuzingatia miongozo iliyopo.
"Asilimia 70 ya mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mwanza yalikosa sifa za kufanya shughuli hizi lakini sasa karibu yote yapo rasmi na tunaendelea kushirikiana nayo kupambana na hali hii.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Jessica Lebba amesema Mkoa wa Mwanza ni wa pili kwa idadi kubwa ya watoto wa mitaani lakini wamejipanga kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Ofisi yake,fawati la ukatili wa kijinsia kuhakikisha elimu ya kuzingatia ulinzi na usalama wa mtoto inatolewa kwa jamii.
"Uzinduzi huu wa leo Mkoa wa Mwanza unakuwa wa kwanza kufanya hivyo hapa nchini,hii ni kuonesha tulivyodhamiria kupambana na hatimaye kutokomeza watoto wa mitaani",Lebba
Mmiliki wa kituo cha DayCare Linah Roman amesema jukumu walilonao hivi sasa ni kuhakikisha wanashirikiana na Serikali kutokomeza hali ya umasikini ndani ya jamii.
Uzinduzi huo uliohudhuriwa na Maafisa ustawi wa jamii kutoka wilaya za Nyamagana na Ilemela ulikwenda pamoja na ugawaji wa vyeti vya kuwatambua kwa baadhi ya vituo vya kulea watoto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.