Serikali imewataka watanzania kuwasomesha watoto wao kwa kuzingatia upeo na kipaji alichonacho na siyo wazazi kuwalazimisha wanachopenda katika familia zao.
Wito huo umetolewa jana na Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Hellen John katika mahafali ya sita ya Shule ya Msingi Gadiz ambapo alisema asilimia kubwa wazazi wamekuwa wakiwasomesha watoto wao bila kuwadadidi au kuangalia kipaji alichonacho kitendo ambacho huchelewesha mafanikio ya mwanafunzi.
John alisema wapo watumishi wengi ndani ya Serikali na mashirika binafsi ambao wameajiriwa kwa taaluma fulani lakini matendo yake na matamanio ya kila siku yanaonyesha kuwa na kipaji fulani tofauti na kazi anayofanya, hivyo alishauri wazazi kuwachunguza na kuwahoji wanachopenda watoto.
“Gadiz ni moja ya shule ndani ya Wilaya ya Ilemela ambayo inatubeba katika mitihani ya kitaifa kutokana na kufanya vizuri na wanafunzi wake kufaulu kwa wastani mkubwa sana, mara zote imekuwa ikishika nafasi ya kwanza au ya pili ngazi ya wilaya na mkoa nafsi ya 15 na 91 kitaifa, hizo ni takwimu za mwaka jana katika mtihani wa darasa la saba.
“Sasa kuna jambo ambalo wazazi tunakosea katika kuwasomesha watoto wetu, mfano halisi leo hapa tumeshuhudia vipaji vya watoto wakionyesha vipaji na umahiri wao katika fani mbalimbali lakini tunashindwa kuendeleza kile anachokipenda badala yake tunawalazimisha kusomea fani ambayo yeye haipendi ispokuwa wewe kama mzazi ndio unaipenda, tunakosea.
“Kila mmoja ajiulize alichokuwa anakipenda na alichosomea ni vitu viwili tofauti, wapo watumishi wenzangi serikalini wanasema wenyewe walikuwa wanapenda fani fulani lakini wazazi wao walilazimisha kusomea fani nyingine, sasa matendo yao ni tofutti na taaluma anayofanyia kazi kila siku naomba mzingatie kile anachopenda mtoto.
“Kumbukuni hivi sasa ili ufanikiwe katika kipaji chochote ni lazima uwe na elimu, isiwe sasa unaona mtoto ana kipaji cha kuimba ukamtoa kwenye masomo ili akaungane na Ali Kiba au Diamond la hasha, hata wale unaoona wanaiimba kuna mambo wanashindwa kuyafanya kutokana na kukosa elimu, ukiwa na elimu ukienda sehemu yoyote unaweza kuongea na mtu yeyote,”alisema.
John aliwataka wazazi kutowaruhusu wanafunzi waliohitimu darasa la saba kusafiri mara kwa mara kutembelea ndugu na jamaa kwani kuna uwezekano mkubwa wa kujifunza mambo mabaya na hata kupata ajali, hivyo aliwahimiza kuendelea kuwalea na kupata masomo ya ziada ya kujiandaa na elimu ya sekondari.
Hata hivyo aliagiza uongozi wa shule zote ndani ya wilaya hiyo kuanza kufikiria mchakato wa ujenzi wa uzio ili kuepusha mwingiliano wa wananchi na wanafunzi ambapo aliamua kuchangia mifuko mitano ya saruji kama sehemu ya uzinduzi wa ujenzi huo.
Akisoma risala ya shule kwa niaba ya Mwalimu Mkuu wa Gadiz, Baraka Maila, Mwalimu wa Taaluma, Sabato Musai alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2012 na imekuwa ikifanya vizuri kwa kila mwaka ambapo alisisitiza kuwa matarajio yao mwaka huu ni kuwa wa kwanza ngazi ya mkoa na kitaifa kuingia 10 bora.
Alisema katika matokeo ya mwaka 2018, walishika nafasi ya tatu kati ya shule 18 ngazi ya wilaya, 15 kati ya 197 ngazi ya mkoa na 91 kati ya 6,726 kitafifa ambapo tayari wamefanyia kasoro zilizokuwapo na kuw ana uhakika wa kufanya vizuri zaidi.
Pamoja na kusoma mafanikio ya shule hiyo, alisema changamoto inayowakabili ni kutokuwa na umeme ambao unafanya wanafunzi kushindwa kujisomea usiku, vile vile aliongeza kutokuwapo na uzio imekuwa ni kero kutokana na wananchi kukatiza shuleni hapo mchana na usiku na mifugo kuharibu miti na miundombinu.
Baadhi ya wanafunzi wakiwamo Asman Mbaraka na Sekei Sabuni walisema wana imani kubwa ya kufaulu kutokana na kufundioshwa vizuri na waliwahi kumaliza mada za masomo yote ambapo zaidi ya miezi sita walikuwa wanafanya majaribio ya mitihani ya miaka iliyopita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.