Mhe. Jenista Mhagama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora amewapongeza watumishi wa umma kwa kujituma katika kuwahudumia wananchi na ku yahakikisha wanamsaidia Mhe. Rais kutimiza ndoto ya kuwafikishia watanzania huduma bora katika nyanja zote.
Ametoa pongezi hizo mapema leo februari 21, 2023 wilayani Sengerema alipokua akizungumza na watumishi wa wilaya hiyo akiwa katika muendelezo wa ziara yake Mkoani Mwanza ambapo anakagua miradi iliyo chini ya wizara yake hususani inayotekelezwa na TASAF.
"Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora inashughulikia malimbikizo ya mishahara maana ni haki yao na wenye madai halali wote watalipwa,na zaidi ya Watumishi laki mbili wamepandishwa madaraja ndio maana hivi sasa tunahakikisha mtu akipandishwa daraja anaanza kupata mara moja mshahara wake mpya na hiyo ndio kiu ya Rais Samia katika eneo hili la utumishi." Waziri Mhagama.
Vilevile, amebainisha kuwepo kwa watumishi wa umma wanaoiangusha Serikali na ndio maana kuna ubadhirifu wa fedha za umma pamoja na usimamizi mbovu wa miradi hivyo amewasihi kuwajibika bila kusubiri kusukumwa kuhakikisha wanafanya kazi kizalendo ili kujenga uchumi wa nchi wa wenyewe.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amempongeza Mhe. Rais kwa kuwajali wanasengerema kwa kutekeleza Miradi ya Kimkakati kama Ujenzi wa Daraja la Kigongo- Busisi ambalo amesema litakapokamilika litasaidia sana kukuza uchumi wa wananchi wa Sengerema na Tanzania kwa ujumla.
Dkt. Angelina Samike, Mjumbe wa baraza Kuu la Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi nchini ametaja changamoto ya uhaba wa watumishi na ametoa ombi kwa Serikali kuendelea kuongeza mshahara ya watumishi ili kuendana na hali ya uchumi kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa.
"Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia maana ametuheshimisha wafanyakazi kwa kutupandisha madaraja, kutupunguzia kodi na kuongeza kima cha chini cha mshahara, kutuongezea Mshahara, ametuboreshea mazingira ya kazi kwa kujenga nyumba za watumishi katika sekta ya Elimu na Afya na tunamwombea kwa Mungu afya njema." Amesema,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.