Waziri Mkuu, Mhe.Kassim Majaliwa wamewaagiza wakurugenzi wote nchini kufanya tathmini kwa kila halmashauri kwa kupitia ahadi zote za Rais Mhe.Dkt. John Magufuli alizozitoa wakati akiomba kura na kuainisha katika makundi matatu iliziweze kutekelezwa kabla ya kurudi kwa wananchi kuomba ridhaa nyingine.
Aliekeleza kuwa ahadi ziwekwe katika mpangilio wa zilizotekelezwa, ambazo zimeanza kutekelezwa na zile ambazo hazijatekelezwa kabisa na kila kundi liainishwe kilichokwamisha au changamoto iliyopo.
Agizo hilo amelitoa jijini Mwanza wakati akifungua mkutano wa 35 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ambapo alielekeza baada ya taarifa ya tathmini hizo kukamilika zinapaswa kutumwa kwake ili Mhe.Rais Magufuli aweze kuzitimiza kabla ya kurejea kwa wananchi kuomba ridhaa kipindi cha pili.
“Rais wetu Mhe. Dkt. Magufuli anafanya kazi kubwa kweli kweli, ikumbukwe mwaka huu ni wa nne tangu ameingia madarakani sasa naomba kila halmashauri ipitie ahadi alizozitoa wakati akiomba kura alipopita halmashauri zetu, fanyeni tathmini na andaeni ripoti inayoonyesha zilizotekelezwa, zinazoendelea kutekelezwa na zile ambazo bado kabisa, katika hilo ainisheni changamoto zake.
“Sote tunajua Mhe.Rais wetu anarudi kwa wananchi ifikapo 2020 kuomba ridhaa tena, hivyo ikiwa atapata ripoti hizi itamsaidia kwa kipindi hiki kujua ahadi zilizobaki na kuzitekeleza, najua tunapozunguka sisi tumebaini moja ya changamoto iliyobaki kubwa ni upungufu wa madaktari na walimu,”alisema.
Majaliwa ambaye katika hotuba yake ilikuwa imejikita kujibu maombi ya risala ya ALAT iliyosomwa na Mwenyekiti wake,Gulamhafeez Mukadam,alisema mwaka huu ni wa uchaguzi hivyo aliwaagiza wakurugenzi kuendelea kuratibu uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuhamasisha wananchi kujiandikisha.
“Endeleeni kuratibu shughuli zote za uchaguzi wa Serikali za mitaa hadi hapo tutakapotangaza vinginevyo, anzeni maadilizi kwani miongozo tumetoa, toeni fursa na haki kwa yeyote mwenye sifa, pia kumbukeni kuwa nimezindua uboreshaji wa daftari la wapiga kura , maboresho yanahusisha na uchaguzi mkuu wa mwakani hivyo mwenye umri wa miaka 17 akajiandikishe maana mwaka kesho atakuwa na miaka 18.
“Katika risala yenu nimesikia maombi mengi sana lakini nianze na hilo la posho kwa madiwani, niseme Rais wetu Mhe. Magufuli ametusihi tuwe na subira kidogo, vivyo hivyo kwa ombi letu la kuinua mgongo kwani kuna timu inafanya tathmini ya suala hilo na itakapomaliza kazi yake pengine tunaweza kupata matunda.
“Kuhusu mgawanyo wa vijiji, kata, wilaya na mikoa, niseme hili nalo Serikali imelisimamisha kidogo kwa sababu tulibaini kuwapo na utitiri wa halmashauri halafu hazina ofisi, wafanyakazi wanarundikana katika ofisi moja, ngoja tuendelee kutatua changamoto zilizopo kwanza ndio tuendelee kufikiria hilo, kikubwa tutaleta fedha za kumalizia majengo yote ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi ili yaweze kumaliziwa,”alisema.
Mhe.Majaliwa aliwataka wenyeviti wa halmashauri na wakurugenzi kusimamia miradi ya maendeleo huku akishangazwa na namna baadhi ya majiji nchini yalivyoshindwa kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo ya kuwaingizia kipato na badala yake wamebaki kulalamika Serikali kuu kuwanyang’anya vyanzo vya mapato.
Alisema Serikali haijafanya kosa kukusanya fedha yote katika mfuko mmoja kwani walifanya tathmini na kuona ni heri fedha ikatunzwa eneo moja na kufafanua kuwa tangu mfumo huo uanze kumekuwepo na miradi mikubwa inayogharimu zaidi Sh. bilioni tano lakini kabla ya hapo kulikuwa na miradi midogo midogo yenye thamani Sh.milioni 700 ingawa mapato yao ni makubwa.
“Tumeelekeza kila halmashauri kubuni mradi wa kimkakati na kutuletea kwa ajili ya kuwapa fedha lakini baadhi ya wakurugenzi wameshindwa kufanya hivyo, hawajui hata kuandika andiko, wakiandika wakileta linatupwa sasa kama hamjui kutetea kile unachokitaka kuanzisha ni heri ukakodi mtu akuandikie.
“Mpaka sasa halmashahuri 17 zimekidhi matakwa katika miradi 22 hawa tunawapa mabilioni ya fedha ili kuanzisha miradi wa kimakakati, awamu ya pili halmashauri 12 zimeonekena kukidhi vigezo nazo zitapewa lakini changamoto ninayoiona ni kutokamilika kwa wakati kwa miradi, watu hawasimamii ipasavyo, wapo wazembe na wanafanya kazi kwa mazoea, jambo lingine ni kutofanya upembuzi yakinifu vizuri.
“Ndiyo maana inafikia hatua Mhe. Rais Magufuli anakuwa mkali kwenu hasa kwa wale wanaofuja fedha, naomba kila halmashauri ipange mipango ya maendeleo, pesa zile zinazokuja zikiwa na maelekezo ya kufanya kazi yake bila kubadilishiwa matumizi, tunahitaji kuona kila kijiji kinakuwa na zahanati,”alisema.
Mhe.Majaliwa aliendelea kusema mbali na kuzitaka halmashauri 10 za mwisho ambazo zilitajwa kwa kushindwa kukusanya mapato na kufikia asilimia 80 zijitathmini na kuona namna ya kutojirudia kitendo hicho katika makusanyo yao ya mwaka 2019/2020 mbapo aliunyoshea kidole Mkoa wa Kigoma ambao halmashauri zaidi ya mbili hazikufikia lengo.
Hata hivyo alisema kilichosababisha Mhe.Rais Magufuli kushindwa kufika katika mkutano na kumwakilisha ni kutokana na kuwa na vikao vizito na wageni kutoka ndani na nje ya nchi vinavyohusu mkutano wa SADC unaotarajiwa kufanyika nchini.
Pia Mhe. Majaliwa alidokeza kuwa Serikali iliamua kumuondoa aliyekuwa katibu mkuu wa ALAT Taifa ambaye hakumtaja jina na kusema alikuwa anafanya mambo ya ovyo ya kuisemea Serikali na kuingia mikataba ya ovyo jambo ambalo lilikuwa halileti sura nzuri kwa Tanzania.
Alisema Serikali iliamua kumtafuta mbadala wake kwa kuzingatia sifa na kumpata Elirehema Kaaya ambaye anafaa kuiongoza ALAT na siyo huyo waliyemuondoa ambapo aliyekuwa ndani ya Tamisemi.
Awali, katika risala Mwenyekiti wa ALAT, Mukadam, alisema moja ya changamoto kubwa inayowakabili ni posho ndogo na kiinua mgongo cha madiwani ambapo aliomba Serikali kuongeza na kufikia asilimia 60 kwani kazi wanayofanya ni kubwa ya kuwahudumia wananchi na kuwatafutia kura wabunge na Mhe. Rais.
Pia aliomba kufanyika kwa mgawanyo wa kata, vijini na mitaa kwani baadhi ya maeneo ni makubwa sana jambo ambalo linaleta changamoto kwa viongozi hao katika kuwahudumia wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.