WAZIRI MKUU ATOA WITO KWA VIJANA KUACHANA NA MATUMIZI NA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) amewataka Vijana wa Kitanzania kuachana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya na badala yake waungane katika kufanya shughuli halali za kiuchumi ili wajiletee maendeleo katika ngazi ya familia, jamii na hata Taifa.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo Juni 30 2024, alipokuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya duniani ambapo Kitaifa yamefanyika Jijini Mwanza kwenye uwanja wa Nyamagana.
"Nitoe wito kwa vijana tuachane na dawa za kulevya na tujikite katika kujenga familia zetu kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kujiletea maendeleo",Waziri Mkuu
Mhe. Majaliwa amesema ili kuondokana na janga la matumizi na biashara ya dawa za kulevya ni lazima kudhibiti kwanza kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari zitokanazo na matumizi ya dawa hizo.
"Ni lazima tuimarishe mikakati yetu ya kukabiliana na mapambano dhidi ya dawa za kulevya na Serikali imejikita katika kutoa elimu ili jamii ifahamu, na tutakwenda kuanzia klabu za mapambano na tutaanzia katika shule za Msingi, Sekondari mpka Vyuo Vikuu kama walivyofanya TAKUKURU",Mhe.Majaliwa
Aidha Waziri Mkuu pia amesema kwa sasa Serikali pia imeongeza upana kidogo na sasa wanagusa nyanja nyingi kwanza wanachi watambue madhara ya matumizi ya dawa za kulevya lakini pia wanawawezesha waliotoka huko (Waraibu) ili waweze kujumuika na wenzao wafanye kazi na waweze kujisimamia.
Kadhalika Mhe. Majaliwa amewataka wananchi waliojitokeza uwanjani hapo kuwa mabalozi wazuri katika kuwaelimisha wale wote ambao hawakupata nafasi ya kushiriki katika maadhimisho hayo kuhusu athari na madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii na Taifa letu kiujumla.
"Dawa hizi, bangi hizi si nzuri, mkawaambie wasikubali kupewa popote unaweza ukapewa cha arusha na utalala hapo hapo ukapotea, hata skanka hii inatisha kwanza jina lenyewe tu linatisha msitumie mtapotea",amesisitiza Mhe.Majaliwa
Pia Waziri Mkuu amesema ni mpango wa Serikali sasa katika kuhakikisha waraibu wote wa matumizi ya dawa za kulevya wanapewa huduma ya matibabu kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali ambapo kwa sasa Serikali inaboresha kwanza huduma za afya kisha waanze kuratibu mpango huo.
"Kwa sasa huduma za matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya zinapatikana katika Vituo 16 nchini na kuwafanya wenye uraibu kupatiwa tiba na elimu".
Kama katika jamii kuna kijana ambaye ni mraibu msisite, mumpeleke katika vituo hivyo lakini pia hata kwa hapa Mwanza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure inatoa huduma ya matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya. Amesema Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa.
Mhe. Majaliwa amewasihi Watanzania kuhakikisha wanaunganisha nguvu kwa pamoja na kwamba aina yoyote ya dawa za kulevya Tanzania sio mahali sahihi kwake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.