Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi mkoani Mwanza Benson Mihayo
kupima viwanja eneo la Fela ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa bandari kavu inayotarajiwa kujengwa katika eneo hilo.
Mhe. Majaliwa amesema hayo leo Oktoba 16, 2022 akiwa eneo la Fela Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya kisasa(SGR) kipande kinachoanzia Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa kilomita 341 kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi Trilioni 3.06 .
Amesema viwanja vilivyopo eneo hilo vikipimwa vitawanufaisha wananchi kwani wenye uwezo wa kifedha wataweza kujengwa hoteli na nyumba za kulala wageni hivyo kujiongezea kipato wao na Taifa kwa jumla.
Aidha, Mhe. Majaliwa amewataka watanzania waliopata nafasi ya kuajiriwa kwenye mradi huo kufanya kazi kwa weledi na bidii huku wakizingatia mafunzo wanayoyapata maana Serikali inawategemea kwa ajili ya kuteleleza miradi mingine.
"Mkifanya kazi kwa weledi nawahakikishia mtaisaidia sana Serikali maana ujuzi mnaoupata kutoka kwa wakandarasi wageni wakiondoka tukianzisha miradi mingine Serikali itawatumia nyie hivyo tutapunguza gharama za kuleta wataalamu wa kigeni kutoka nje ya nchi,"ameongeza.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema mradi huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 14.12 ni mhimili mkubwa na thabiti katika ukuaji wa uchumi wa taifa maana ukikamilika utaleta mapinduzi katika sekta za viwanda, kilimo, ujenzi, ufugaji, usafirishaji, madini pamoja na utalii.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Amina Lumuli amebainisha kwamba mradi huo umekuwa na mafanikio mengi kwa watanzania kwani hadi Septemba 30, 2022 ulikuwa na jumla ya wafanyakazi 5,897 kati ya hao 5,384 sawa na asilimia 91.3 ni watanzania na 513 sawa na asilimia 8.7 ni raia wa kigeni.
Ameongeza kuwa TRC imeendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa wataalamu wake mbalimbali, mafunzo hayo yamekuwa na tija sana kwani zaidi ya wataalamu 40 wanashiriki moja kwa moja kwenye ujenzi wa mradi wa SGR.
" Mradi huu ukikamilika utakuwa na faida mbalimbali ikiwemo kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kupunguza muda wa safari mathalani kutoka jijini Dar es Salaam hadi Mwanza kutoka masaa 18 hadi 20 ya awali hadi nane, vilevile utachochea uanzishwaji wa miji midogo katika sehemu zinazojengwa stesheni ambazo zitakuwa kivutio kwa wananchi.
" Pia utapunguza gharama za usafirishaji mizigo kati ya asilimia 30 hadi 40 na kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuhimili ushindani, utachochea uanzishwaji wa viwanda maeneo mengine ya nchi kutokana na uwepo wa uhakika wa usafirishaji wa malighafi na bidhaa,"ameeleza.
Mhe. Majaliwa yuko Mkoani Mwanza tangu Oktoba 15 ,2022, kwa ziara ya siku nne ya kikazi lengo likiwa ni kukagua maendeleo ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali pamoja na kukutana na wananchi ili kuwaeleza kuhusu miradi mbalimbali ambayo serikali ya awamu ya sita inaitekeleza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.