Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amewataka wadau na wavuvi kuacha mara moja tabia ya Uvuvi Haramu kwani vitendo hivyo vina madhara makubwa katika Uendelezaji wa sekta ya Uvuvi nchini.
Wito huo umetolewa mapema leo (Novemba 17, 2022) jijini Mwanza na Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa niaba ya Mhe. Waziri Mkuu katika Mkutano uliowakutanisha viongozi wa Serikali na wadau wa Sekta ya Uvuvi kutoka Kanda ya Ziwa Victoria uliolenga kuwajengea uwezo dhidi ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kwa Ukuaji wa Uchumi wa Buluu.
Amebainisha kuwa, Utafiti wa kisayansi uliofanywa mwaka 2021 umeonesha kuwa samaki aina ya Sangara wamepungua kwenye ziwa Victoria kwa asilimia 50 na kwamba wengi wapo kwenye hatari ya kutoweka kutokana na uvuvi haramu na Uharibifu wa mazingira hali inayotishia uwepo wa viumbe hao kwa miaka ijayo.
Aidha, ameelekeza pia Wizara hiyo kuandaa Mikutano ya mara kwa mara ya kuwakutanisha wadau kujadili katika ukuzaji wa sekta hiyo, uboreshaji wa Uvuvi wa samaki wa vizimba kwa kuwaongezea uelewa wanaojihusisha ili kujenga uendelevu na kuwataka maafisa Uvuvi kudhibiti uvuvi haramu kwa kufanya doria ya mara kwa mara.
Vilevile, Amewaagiza Wizara ya TAMISEMl kusimamia kikamilifu maeneo yenye Rasilimali za Uvuvi, kutenga fedha asilimia tano ya mapato yanayotokana ma sekta hiyo kulingana na miongozo na kamati za Ulinzi za Vijiji na Kata kufanya doria kwa wavuvi haramu na kuwachukulia hatua stahiki.
"Hakuna haki isiyoambatana na Wajibu, Sekta binafsi hakikisheni mnakuza sekta hii kwa kufuata sheria za uvuvi na kwenye vikundi vyenu jiimarisheni kwenye uhamasishaji wa uendezaji wa uvuvi mkubwa ili kukidhi mahitaji ya viwanda na vilevile epukeni kuchakata samaki wachanga kwani tabia hiyo inamaliza samaki ziwani. " Waziri Mkuu.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wavuvi kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria na kanuni ili pamoja na kufanya uvuvi unaokubalika waweze pia kuhifadhi mazingira ya mazalia ya viumbe hai wanaopatikana kwenye bahari, maziwa makuu na madogo na kufanya kuwa endelevu ili kuchochea biashara ya uvuvi.
Awali, amesema kuwa katika mwaka 2021 zaidi ya wananchi Laki moja na elfu Tisini na Moja walijishughulisha moja kwa moja na shughuli za uvuvi na kwamba asilimia 53 wametoka kwenye ukanda wa ziwa Victoria hivyo mchango wa ziwa hilo ni mkubwa sana ambapo wadau wote wanalazimika kuendelea kulinda rasilimaji hiyo muhimu kwa pamoja.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdalah Ulega (Mb) amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 katika ukanda wa Afrika zenye utajiri mkubwa wa maji ambayo ni fursa kubwa ya kukuza uchumi wa wananchi kupitia shughuli za uvuvi na kwamba inachangia Pato la Taifa kwa asilimia 1.8.
"Ziwa victoria pekee lina takribani tani milioni 3 za samaki na maji ya kitaifa ya bahari ya Hindi yanakadiriwa kuwa na Mazalia ya zaidi ya tani laki 1 na hivyo wavuvi wadogo huchangia takribani zaidi ya asilimia 93 na wavuvi wadogo zaidi ya laki moja wamejihusisja moja kwa moja kwenye uvuvi kupitia maji ya asili." Amesema Mhe. Ulega.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amebainisha kuwa wananchi zaidi ya Milioni moja na nusu mkoani humo wanajihusisha na shughuli za Uvuvi ambapo sekta hiyo imekua ikitoa mchango mkubwa sana kwa wananchi hao kwa kuwapatia ajira, uchumi na kipato cha kila siku.
Aidha, amebainisha kuwa Mkoa huo unaendelea kusimamia kikamilifu Ukusanyaji wa mapato kwenye sekta hiyo ili kusaidia ukuzaji wa uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo nyeti kwenye ukanda wa Ziwa Viktoria ili kufikia malengo ya kukusanya Bilioni 5.6 kwa mwaka 2022/23.
"Sekta ya Uvuvi imeendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa Halmashauri zinazozunguka ziwa Victoria. Mathalani katika mwaka 2021/22 kiasi cha Bilioni Tatu na Milioni Mia nne zilikusanywa na Halmashauri za Mkoa wa Mwanza kutokana na ushuru wa mazao ya uvuvu, leseni za Uvuvi na vyombo vya uvuvi." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi Dkt.Rashid Tamatamah aliwasilisha Changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo kuwa ni pamoja na Upungufu wa Mazao ya Uvuvi, Uvuvi haramu, Utoroshaji wa Mazao ya Uvuvi pasipo kulipia Kodi na Uharibifu wa Mazingira na akatumia wasaa huo kukemea vitendo hivyo pamoja na hali ya kipato duni inayowakabili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.