Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) ametaka kuwepo na nidhamu nzuri ya matumizi ya fedha za Miradi ya Maendeleo akitoa mfano wa kuigwa Wilaya ya Ukerewe Kisiwa cha Irugwa.
Akizungumza leo Kisiwani Irugwa wakati wa ukaguzi wa vyumba vya madarasa 6 shule ya Sekondari Irugwa vilivyogharimu Tshs milioni 120 na kutumika Tshs milioni 119, Mhe. Majaliwa amesema kwa jiographia ya Kisiwa hicho na nidhamu ya matumizi ya fedha hizo wahusika wote wanastahili pongezi.
"Leo nawapa zawadi ya Tshs Milioni moja mkagawane kwa nidhamu mliyoonesha maana natambua changamoto ya kuleta Vifaa hapa vya ujenzi lakini bado mmetumia fedha vizuri na chenji kubaki, Viongozi wengine nataka wapate ujumbe huu." Amesisitiza Waziri Mkuu.
Mhe. Majaliwa amebainisha kuwa bado kuna changamoto sana ya matumizi ya fedha za Serikali zinazolengwa kuwaletea Maendeleo wananchi na kusisitiza hatakuwa na huruma Kwa Viongozi wenye tabia hizo.
Aidha, Waziri Mkuu ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kisiwani Irugwa kilichogharimu Tshs milioni 500 na kuahidi kuletwa kiasi cha Tshs milioni 270 kwa ajili ya kukiboresha Kituo hicho kiwe na matibabu yote ya msingi likiwemo jengo la Mama na Mtoto.
Akijibu hoja ya Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe Denis Mwila kuhusiana na ubabaishaji wa Mkandarasi wa barabara za ndani mjini Nansio kampuni ya Inter Country inayomilikiwa na Mazoa Nyakilagani, Mhe. Majaliwa ameagiza Mkandarasi huyo kufika Ofisini kwake Dodoma wiki hii ili kujibu tuhuma za kuzembea kukamilisha Mradi huo.
Kuhusu kero ya usafiri wa Mitumbwi Kisiwani humo Mhe. Majaliwa amewaahidi Wakazi hao kulibeba suala hilo na kwenda kulifanyia kazi ili wapate kivuko cha uhakika.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amesema Mkoa huo umeendelea kunufaika na Miradi mbalimbali ya Maendeleo kuanzia Sekta ya Afya, Elimu na Miundombinu.
"Mhe. Waziri Mkuu Kisiwa cha Irugwa kipo mbali sana kutoka mjini Nansio na wakazi wa huku huduma za haraka kwao wanazipata Mkoani Mara ambako ni karibu hivyo kuwaletea huduma zote za msingi hapa kutawapunguzia usumbufu," amesema Mkuu wa Mkoa.
Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa anaendelea na ziara yake mjini Mwanza kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Stendi ya m
Mabasi ya Nyegezi na ujenzi wa Meli mpya Mv Mwanza Hapa Kazi tu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.