Serikali imesema itaendelea kushirikiana na taasisi za dini hasa zinazojikita kutoa huduma za jamii ikiwemo afya ili kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya bora likiwemo Kanisa Katoliki.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 16, 2022 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wakati akizungumza na wananchi pamoja na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando(BMC) baada ya kuzindua jengo la kutoa huduma za macho hospitalini hapo lililogharimu Sh bilioni 3.7 kati ya hizo ujenzi Shilingi bilioni 2.4 na vifaa bilioni 1.3.
Mhe. Majaliwa amesema uwepo wa hospitali ya BMC ambayo inatoa huduma za juu kabisa za kibingwa kama zinazotolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni faraja kwa wananchi wanaoishi Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwani Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele kutoa huduma katika sekta ya Afya pamoja na sekta zingine.
Ameongeza kuwa, kwa miaka mingi Kanisa Katoliki limekuwa likijishughulisha na ustawi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla wake na kuhakikisha linamstawisha mwanadamu kiroho na kimwili linamiliki vituo vidogo vidogo vya kutolea huhuma za afya zikiwemo zahanati jumla 387.
"Idadi hiyo inajumuisha hospitali za rufaa za ngazi ya mikoa ambazo zipo kwenye mikoa tisa, hospitali za wilaya 33 vituo vya afya 103 na zahanati 223 hakika mkakati huu wa kuendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kutujengea vituo karibu unafaa kupongezwa sana kwani mchango wa Kanisa Katoliki katika eneo la afya ni mkubwa sana,"ameeleza.
“Ninapozungumzia mchango wa Kanisa Katoliki katika eneo la afya ni mchango uliokithiri kwa serikali maana nalo linaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kutoa huduma za afya kwa wananchi wake, hospitali hii inatoa hudumza za kutosha kwenye maeneo yote,”amesema Mhe. Majaliwa na kuongeza
“Sasa imejiimarisha zaidi kwenye maeneo ya saratani na macho, hivyo wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa hawatalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 100 kwenda jijini Dar es Salaam kufuata huduma za saratani Ocean Road au kwenda CCBRT kufuata huduma za macho,”ameongeza Mhe.Majaliwa.
Awali akimkaribisha Mhe. Majaliwa kuzungumza na wananchi waliofurika hospitalini hapo, Naibu Waziri wa Afya, Mhe.Dkt. Godwin Mollel amesema kukamilika kwa jengo hilo kutakuwa ni faraja kwa watu wenye matatizo ya macho kwa wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa kwani asilimia 4 ya watanzani wana matatizo ya macho na zaidi ya asilimia 90 ya matatizo hayo yanatibika.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya BMC, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Renatus Nkwande ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kufanya maboresho ya huduma za macho kwa haraka na kasi kubwa kwani zaidi ya miaka 40 tangu hospitali hiyo ianzishe walikuwa na daktari bingwa wa macho mmoja tu ambaye alikuwa anahudumia kanda nzima sasa wapo madaktari bingwa sita wawili kati yao ni madaktari bingwa bobezi wa macho.
“Kukamilika kwa jengo hili pamoja na vifaa vya kisasa kunasababisha tuone changamoto ya upungufu wa rasilimali watu, hivyo tunaiagiza hospitali pamoja na Chuo Kikuu cha CUHAS waanze kufikiria namna ya kuanza kuzalisha wataalamu wa afya ya macho hapa hapa bugando maana wataalamu bingwa na bobezi wanao hapa hospitalini, vifaa tiba wanavyo, wagonjwa wapo, wahisani wapo na serikali nayo ipo kwa ajili ya kutoa miongozo na kutusaidia,”ameagiza Askofu Nkwande.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi akisoma taarifa ya siku ya macho duniani kwa Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema Takwimu za Shirika la Afya Duniani zimeonyesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu wenye ulemavu wa kutokuona na upungufu wa kuona iwapo kusingechukuliwa jitihada mbalimbali kwani zaidi ya asilimia 75 ya matatizo yote ya kutokuona yanayoikabili dunia yanachangiwa na sababu zinazoweza kuzuilika ama kutibika kwa gharama nafuu.
“Kwa kutambua hilo Tanzania inaandaa na kutekeleza mpango mkakati wa afya ya macho kwa vipindi tofauti, aidha sekta ya afya imeendelea kuimarisha rasilimali watu, miundombinu, vifaa na vifaa tiba kwa utolewaji wa huduma za macho ikilinganishwa na mwaka 2003 tulipoanza mkakati wa dira ya mwaka 2020 na uzinduzi wa jengo hili leo ni mchango wa serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata afya ya macho,”amesema Profesa Makubi.
Mkurugenzi wa BMC Dkt. Fabian Massaga amesema jengo hilo ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 linakidhi viwango vya kimataifa na kitaifa kwani linauwezo wa kutoa huduma za kliniki, vipimo, huduma ya miwani, chumba cha upasuaji, wodi zenye vitanda 50, ukumbi wa mikutano na ofisi za wafanyakazi huku akibainisha kwamba vifaa vyote vya tiba na samani za ofisi zimekwishanunuliwa.
“Ujenzi wa jengo hili ulianza rasmi Machi, 2, 2021ulikamilika Juni 12, 2022 kliniki hii imeanza kutoa huduma rasmi Agosti 15, 2022 hadi sasa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa ukilinganisha na kliniki ya awali ambapo wastani wa wagonjwa ilikuwa ni 70 kwa siku sasa ni wastani wa wagonjwa 120 kwa siku ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 42 ndani ya miezi miwili,”amesema Dkt. Massaga.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amefafanua kwamba mkoa huo una jumla ya vituo 457 vya kutolea huduma za afya kati ya hivyo 29 vinamilikiwa na taasisi mbalimbali za dini na kwamba matamanio ya mkoa huo ni kuwa kitovu katika kutoa huduma za afya za kibingwa ambapo ametoa wito kwa taasisi nyingine za dini kuwekeza katika sekta ya afya.
BMC inamilikiwa kwa ubia na serikali pamoja na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.