Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amezitaka Halmashauri zote kutunga sheria ambazo zitakua ni rafiki kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa kuhakikisha wanashirikiana na wadau katika mapendekezo ya utungaji wa sheria ndogo ndogo.
Mhe. Majiliwa ameyasema hayo leo Mei 9, 2023 alipowasili Jijini Mwanza kwa ajili ya ufunguzi wa Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wachimbaji wadogo wa Madini (FEMATA) ambalo limefanyika katika ukumbi wa Rock City Mall.
" Nawaelekeza Mameya wa Halmashauri nyie ndio mnaotunga sheria ndogo muwe mnahakikisha mnawashirikisha wadau katika mapendekezo ya utungaji wa sheria ndogo ili msiwe mnatunga sheria ambazo zitakuwa zinawaumiza watumiaji wa sheria hizo," Amesema Mhe. Majaliwa
" Sekta ya madini imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kongamano hili lina fursa kubwa kwetu katika kuzitoa changamoto zetu ili kuongeza tija katika kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya madini," Ameongeza Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali.
Aidha Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Madini Mhe. Dkt Dotto Biteko amemuahidi Mhe. Majaliwa kuwa Wizara yake itaendelea kupokea na kusimamia mikakati inayotolewa na serikali.
" Mhe. Waziri Mkuu nakuahidi kuwa Wizara itaendelea kupokea na kusimamia mikakati inayotolewa na serikali ili kuhakikisha inaongeza kasi katika kuchangia maendeleo nchini," Amesema Mhe. Dkt. Kiruswa
Pia Mhe. Adam Malima Mkuu wa Mkoa wa Mwaza ameiomba Wizara ya Madini na Shirikisho la vyama vya wachimbaji wadogo wa Madini (FEMATA) kuja kufanya kongamano lijalo la Mwaka 2024 mkoani humo
" Mhe. Mgeni rasmi kama kauli mbiu yetu inavyosema kwamba amani iliyopo Tanzania itumike kuwa fursa ya kiuchumi na Tanzania kwa kitovu cha biashara ya madini Afrika tunaiomba serikali iunde chombo maalum ambacho kitashughulika na suala la amani ili kukuza uchumi," Amesema Ndg. John Binna,Rais wa FEMATA
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amefungua kongamano hilo la Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wachimbaji wadogo wa Madini (FEMATA) ikiwa ni maagizo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.