WEKEZENI KATIKA MICHEZO NI AJIRA YA UHAKIKA KWA WANAMICHEZO-RC MAKALLA
*Awashauri wenye shule kuvibaini vipaji na kuweka mikakati ya kuviendeleza
*Asema wanamichezo sasa ndiyo wanaotamba Duniani kwa kupata vipato vikubwa
Wamiliki wa shule na wadau wa michezo kwa ujumla Mkoani Mwanza wameshauriwa kufanya uwekezaji wa kweli katika sekta ya michezo kwa kuvibaini vipaji na kuweka mikakati ya kuviendeleza.
Akizungumza Alhamisi hii kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana mara baada ya mchezo wa fainali soka la wanawake ligi ya mabingwa mkoa ngazi ya Taifa kati ya Fountain Gate na Mwanga FC,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA.Amos Makalla amesema mafanikio katika michezo ni matokeo ya uwekezaji mzuri kwa kuvibaini vipaji vya wachezaji tangu hatua za awali.
Makalla ambaye amesakata kabumbu miaka ya nyuma amebainisha Ulimwemguni hivi sasa wanaotamba kwa vipato vikubwa ni wanamichezo mbalimbali ambao ni matunda ya kuandaliwa tangu wakiwa na umri mdogo.
"Tumeshuhudia mchezo mzuri wa fainali soka la wanawake umri wa wachezaji hawa ndiyo sahihi kuhakikisha wanawekewa mikakati kamambe ya kuendelezwa,mwanangu kasoma shule hii ya Fountain Gate sasa hivi yupo kwenye majaribio huko Hispania," amefafanua CPA Makalla
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mpambano huo wa fainali, amewapongeza mabingwa wa michuano hiyo timu ya Fountain Gate kutoka Dodoma kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwanga ya Kigoma,matokeo ambayo yamewapa tiketi ya kucheza ligi daraja la kwanza msimu ujao.
Michuano hiyo ya Ligi ya mabingwa mkoa kwa upande wa wanawake ngazi ya Taifa,imeshirikisha jumla ya Mikoa 19 huku michezo hiyo ikirindima kwenye viwanja vya Nyamagana na CCM Kirumba.
Miongoni mwa mashuhuda wa mchezo huo wa fainali ni pamoja na Rais wa Shirikisho la soka nchini,TFF Wallace Karia,Mwenyeki wa kamati ya soka la Wanawake nchini,Hawa Mniga, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mwanza,MZFA Vedasto Lufano na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mhe.Stanslaus Mabula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.