Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewakumbusha wakazi wa Mkoa huo kuitumia vizuri wiki ya Kitaifa ya magonjwa yasiyoambukiza ili kujitambua mapema afya zao.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mh. Hassan Masala akizindua rasmi leo wiki hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa kwenye uwanja wa CCM Kirumba,amesema kasi ya magonjwa yasiyoambukiza imekuwa kubwa kutokana na watu wengi kutozingatia kanuni za afya likiwemo suala la kujichunguza mara kwa mara.
"Nitumie nafasi hii kuwakumbusha ndugu zangu ule usemi wa kinga ni bora kuliko tiba,haya magonjwa yamekuwa ni mzigo wa gharama na kusababisha nguvu kazi ya Taifa kupotea kutokana na vifo au kazi kuzorota,tuna kila sababu ya kuelimika kuanzia aina ya ulaji wa vyakula usiofaa na tufanye mazoezi" amesema Mhe.Masala
Ameendelea kusema wiki hiyo itakuwa ni msaada mzuri kwa Wananchi watakaofika uwanjani hapo na kukutana na Wataalam wa Afya ambao watawafanyia vipimo na kupewa elimu.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa magonjwa yasiyoambukiza,ajali na afya ya akili kutoka Wizara ya afya Dkt.James Kiologwe amebainisha Wizara yake inaendelea kuwa mstari wa mbele kuelimisha umma kwa njia mbalimbali ikiwemo kama hii inayofanyika Mkoani Mwanza lengo likiwa watu watambue umuhimu wa kinga mapema.
"Watu wengi bado wanaishi wakiwa na maradhi kama shinikizo la damu,kisukari na saratani bila kujitambua mapema na wanapoanza kuumwa ndipo wanagundulika na matatizo hayo hali ambayo inawaletea taharuki na hofu" amesisitiza Dkt.Kiologwe
Uzinduzi wa wiki ya Kitaifa ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo kilele chake itakuwa Novemba 12 mwaka huu, imeanza kwa Wananchi wa Mwanza kushiriki mbio pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo soka,mpira wa pete na kikapu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.