Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amezitaka Halmashauri zote mkoani humo kuiga mfano wa Halmashauri ya Wikaya ya Misungwi na Magu kwa kupanda miti katika maeneo yote ya shule ili kurejesha Uoto wa asili na kusaidia katika kukabiliana na hewa ya ukaa.
Ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa vyumba 44 vya Madarasa vyenye thamani ya shilingi milioni 880 katika shule ya Sekondari Idetemya ambapo pamoja na mambo mengine amebaini hali ya kuridhisha katika upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira shuleni hapo.
Aidha, ametoa rai kwa Uongozi wa Halmashauri hiyo kuongeza eneo kwenye shule mpya ya Jitihada ili kusaidia shule hiyo kuwa na uwezo wa kupanuliwa kwa kuongeza miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na madarasa kutokana na shule hiyo kuwa katika maeneo ya mjini yenye ongezeko kubwa la watu.
"Hamuwezi kuwa na shule mpya leo hii yenye hekari sita pekee, fanyeni jitihada kuongeza eneo ili kuiwezesha kumudu ongezeko la wanafunzi kwa mipango ya sasa na baadae na msitegemee kuanzisha shule mpya mbali kwani zitakua na gharama ya usafiri kwa wazazi katika kuhakikisha watoto wao wanafika shuleni" amesema Malima.
Kwa upande wake katibu Tawala Mkoa, Ndugu Balandya Elikana amewataka wazazi kuwapeleka watoto shule wakaanze kidato cha kwanza kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameshawajengea madarasa na miundombinu mingine.
"Ujenzi wa vyumba hivi vya madarasa umeenda sambamba na matengenezo ya Samani kwa wanafunzi ambapo Seti za viti na meza 1760 zimetengenezwa na wanafunzi 1767 watanufaika." Amesema Mkuu wa Idara Mipango na Uratibu, Peniel Titus.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.