Wizara ya Mifugo na Uvuvi imevikumbusha vyama vya Ushirika kufanya kazi kwa weledi ili viwe chachu ya kuinua uchumi kwenye Sekta hiyo ambayo Serikali inazidi kuboresha mazingira yao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega amesema hayo leo Jijini Mwanza kwenye Maabara ya Samaki wakati wa hafla fupi ya utiliaji saini baina ya Chama cha Ushirika cha Uvuvi cha Bukasiga na Ushirika wa Wataalamu wajasiriamali kutoka Chuo cha kilimo Sokoine SUGEKO ,amebainisha kuwa Serikali imeongeza zaidi ya Shs Bilioni 100 kwenye Sekta ya Uvuvi lengo likiwa kuongeza nguvu ya kuwainua wavuvi ili wafanye shughuli hiyo kisasa zaidi.
"Serikali ya awamu ya Sita katika bajeti yake ya mwaka 2022-23 ilitenga Shs bilioni 60 kwa ajili ya Uvuvi na bilioni 40 zilienda kwa wafugaji huku bilioni 20 zikilenga ufugaji wa kisasa wa samaki" amefafanua Naibu Waziri.
Aidha mwaka huu amesema wavuvi watakopeshwa boti za kisasa za Uvuvi ili lengo litimie la wavuvi kujipatia kipato zaidi.
Ameongeza kuwa Serikali imeweka benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB ili sasa watu wa Sekta hiyo kujiaminisha na shughuli zao kutokana na kuwa na uhakika wa kukopeshwa fedha tofauti na miaka ya nyuma Benki zilikuwa zikihofia kupoteza fedha zao.
"Kutokana na kasi ya kumletea maendeleo mwananchi inayo onesha Serikali sisi kama Mkoa tumeendelea kuhimiza na kutoa elimu kwa vikundi maalum kuchangamkia fursa ya Uchumi wa bluu kwa kufuga samaki wa Vizimba,mradi ambao umeonesha kuwa na tija" Emil Kasagara kaimu Katibu Tawala Uchumi na Uzalishaji
Mbunge wa Ukerewe Mh.Joseph Mkundi ameiomba Serikali kuipa kipaumbele Wilaya ya Ukerewe katika mkakati wa kuwainua wavuvi kiuchumi nchini kutokana na Wilaya hiyo watu wake kujishughulisha na Uvuvi.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilikikopesha Chama cha Ushirika cha Bukasiga kutoka Ukerewe Shs Milioni 260 mwaka 2020 kwa ajili ya mradi wa ukaushaji dagaa,hata hivyo baada ya kutokea hali ya kusuasua wa mradi huo, Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo cha Kilimo Sokoine wameingia mkataba wa kuendesha mradi huo kwa kipindi cha mpito na kuchukua deni la mradi huo Shs Milioni 106,000,000.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.