ZAIDI YA BILIONI 3 ZAJENGA HOSPITALI YA WILAYA MISUNGWI, KUWAONDOLEA WANANCHI ADHA YA KUTEMBEA UMBALI MREFU
*RC Makalla amshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwenye Miradi*
*Awataka Halmashauri kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo kwa hiyari*
*Awaagiza watumishi wa Afya kufanya kazi kwa bidii kutoa huduma*
Leo Novemba 06, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amekagua Ujenzi wa Hospitali ya Misungwi inayojengwa kwa zaidi ya Bilioni 3 na amewaagiza wasimamizi wa mradi huo kukamilisha kwa wakati ifikapo Disemba 31, 2023 ili huduma zinazosubiriwa zianze kutolewa.
Mhe. Makalla amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo jinsi gani anawajali wananchi wa Misungwi kwa kuwajengea hospitali hiyo kwenye kijiji cha Iteja ambapo ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha.
Amebainisha kuwa mbali na ujenzi huo, serikali inaleta Gari la kubeba wagonjwa na kwamba pamoja na vifaa tiba vya kisasa ili kuwahakikishia wananchi hao wapatao zaidi ya laki 4 huduma bora na za kisasa za afya.
"Rais Samia amefanya kazi kubwa sana Misungwi, nimeona na kuthibitisha ujenzi wa kiwango kikubwa sana wa majenga zaidi ya 14 kwenye hospitali hii pamoja na vifaa tiba kama mashine ya Mionzi sasa naomba sote kwa pamoja tushiriki katika kukamilisha ujenzi huu." Amesema Mhe. Makalla.
Aidha, Makalla ametumia wasaa huo kuitaka Halmashauri kuwalipa fidia wananchi wazalendo waliopisha ujenzi wa hospitali hiyo kwa hiyari katika kuhakikisha wanasogezewa huduma ambayo awali walilazimika kuifata kwenye kituo cha Afya Mitindo kilicho umbali wa Kilomita 8.
Mhe. Makalla amehitimisha ziara yake wilayani Misungwi kwa kukagua ujenzi wa shule mpya ya msingi Mwabebeya kwenye kijiji cha Nyang'hmango iliyojengwa na mradi wa kuimarisha elimu ya Awali na Msingi 2022/23 (BOOST) kwa zaidi Milioni 540 ambapo ameipongeza halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri.
"Mmefanya kazi kubwa, tuliambiwa madarasa haya yakamilike kabla ya mwezi wa 12 lakini nyie mmekamilisha kabla ya wakati, hongereni sana na kwa pamoja tumshukuru sana Rais Samia kwa kutuletea fedha nyingi kujenga Miundombinu hii na mingine kama vile miradi ya SEQUIP kwa upande wa sekondari." Mhe. Makalla.
Halikadhalika, amesema hakuna sababu ya mtoto kuzurula mtaani hivyo wazazi wakikishe watoto wanaandikishwa na kujiunga na shule hiyo ambayo inakwenda kuondoa adha ya msongamano kwenye shule zingine ndani ya kata na kijiji hich na akamuagiza Mkurugenzi mtendaji kuharakisha mchakato wa kumpata Mwalimu Mkuu kwenye shule hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.