ZAIDI YA MILIONI 900 ZA TASAF ZAJENGA SHULE YA SEKONDARI IGOGWA- ILEMELA
*Miradi 12 kati ya 20 ya Miundombinu Ilemela yatekelezwa shuleni hapo*
*Watoto wapata shule jirani na mitaa wanayoishi*
*Yasaidia kupandisha mahudhurio ya wanafunzi darasani*
*Jamii yapewa wito kutunza miundombinu ya Shule hiyo*
Siku ya tatu ya kikao kazi kilichowakutanisha waratibu wa TASAF, wahasibu, Maafisa manunuzi na Maafisa ufuatiliaji kutoka Wilaya za Mkoa wa Mwanza imewafikisha timu hiyo kwenye mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Igogwa wilayani Ilemela inayotekelezwa kwa zaidi ya Milioni 900.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi huo Mratibu wa Mpango wa TASAF wa Manispaa ya Ilemela Leonard Robert amesema katika ujenzi wa shule hiyo kuna utekelezaji wa miradi 12 ya Miundombinu kati ya 20 inayotekelezwa kwenye Manispaa hiyo kwa zaidi ya Bilioni 1.9.
Robert amebainisha kuwa pamoja na ujenzi wa jengo la utawala, madarasa 4, maabara za sayansi 2, maktaba, nyumba ya walimu ya familia 2, mabweni 4 pamoja na miundombinu ya maji, mradi huo umepata pia samani kwenye maeneo ya mradi.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kuelekeza zaidi ya Milioni 908 kutujengea miundombinu ya shule yetu ambayo inahusisha madarasa, maabara za sayansi, mabweni, nyumba ya Walimu lakini sio hayo tu bali watoto 40 wamepata pia ufadhili chini ya mradi wa TASAF," amesema Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Athanas Manyika.
Vilevile, Mwalimu Manyika amebainisha kuwa awali watoto walitembea zaidi ya KIlomita 20 kwenda na kurudi kupata elimu kwenye shule ya Sekondari Shibula lakini kwa sasa wamepata shule jirani na mitaa inayozunguka shule hiyo mpya na kufanya mahudhurio ya wanafunzi darasani kuwa mazuri.
Aidha, amebainisha kuwepo kwa juhudi za dhati zinazofanywa na Halmashauri katika kuhakikisha wananchi wanapata fidia ya ardhi kwenye eneo hilo ili kuongeza eneo la shule na kufanya shule hiyo kuwa kwenye mazingira nadhifu na salama wawapo shuleni na bwenini.
Naye, Bi. Anastansia Mpanda, Mtendaji wa mitaa ya Igongwa na Kimanilwentemi amesema wananchi wanaitiilkia wito na wanachangia nguvu kazi kwa ari kwenye ujenzi na kwamba wanaishukuru Serikali kwa kuwaletea miradi ya jamii.
Halikadhalika, Mwenyekiti wa mtaa wa Igogwa James Kavera amebainisha kuwa wananchi wa mtaa wake wamekua bega kwa bega kwa Serikali kuhakikisha wanachimba msingi, wanasomba maji na mchanga kwenye msingi ili kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huo.
Mgawa Maswa, Mgane anayelea watoto wanne ameishukuru Serikali kwa kujenga shule ya Sekondari na amebainisha kuwanufaisha watoto wake na wengine kupata fursa ya elimu na hakuacha mbali mradi wake wa ufugaji mbuzi unaoimarishwa kupitia fedha za uhaulishwaji kutoka TASAF.
Ziara ya wataalam hao wilayani Ilemela imehitimishwa kwa timu kuzungumza na walengwa wa TASAF kwenye mtaa wa Igogwe katika kata ya Igogwe ambapo wanufaika hao kwa pamoja wameishukuru Serikali kwa kuwaletea mradi wa shule pamoja na miradi mingine ya huduma za jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.