Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 82 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika mpango wa kunusuru kaya maskini awamu tatu ndani ya Halmashauri nane za Mkoa wa Mwanza ambapo wanufaika zaidi ya elfu 51 wamenufaika na fedha hizo.
Akizungumza katika kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa mpango, Mkuu wa Wilaya ya Nyamgana Mhe. Amina Makilagi alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiendeleza TASAF kwa mafanikio makubwa.
Mhe. Makilagi amesema TASAF imekuwa na mafanikio makubwa katika awamu ya sita kwani idadi ya miradi ya maendeleo na wanufaika imeongezeka ukilinganisha na kipindi cha hapo nyuma.
Kupitia taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa TASAF awamu ya tatu kipindi cha pili, iliyosomwa na Mratibu wa TASAF Mkoa wa Mwanza Bi. Monica Mahundi amesema Mwanza ni miongoni mwa Mikoa inayotekeleza miradi ya kupunguza umaskini awamu ya nne (TPRP IV) ambapo jumla ya gharama za miradi hiyo ni shilingi 19,695,345,100.12 inatekelezwa.
“Hadi sasa, jumla ya miradi 242 inatekelezwa miradi 73 ni ya afya na 169 ni ya elimu. Miradi 175 imekamilika na miradi 67 inaendelea na utekelezaji”. Bi. Mahundi.
Kadhalika, Bi. Mahundi amesema Mkoa wa Mwanza unatekeleza Programu ya kuweka akiba na kukuza uchumi kupitia Mpango wa kunusuru kaya Maskini. Hadi sasa, Mkoa umeunda vikundi vipatavyo 3,729, kati ya hivyo vikundi 3,729 vimesajiliwa kwenye Mfumo.
Kuhusu mafanikio Bi. Mahundi amesema Walengwa 42,804 wameanzisha shughuli za kujiongezea kipato ikiwa ni pamoja na biashara ndogo ndogo, kilimo na ufugaji. Walengwa 15,608 wameweza kujenga nyumba na kuboresha makazi.
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ni mojawapo ya mradi katika Programu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Awamu ya Tatu (TASAF III) ambao ulizinduliwa Mkoani Mwanza Oktoba 2014 na utekelezaji wake ulianza Julai 2015.
Mpango huo una lengo la kuziwezesha Kaya maskini kuongeza kipato, fursa na kuongeza ufanisi katika matumizi ya chakula, afya na elimu. Kimkoa Mpango huu unatekelezwa katika Wilaya zote 7 kwa wanufaika wanufaika 51,944.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.