ZAIDI YA WANANCHI ELFU 23 WA KATA YA KAGUNGULI UKEREWE WAPATA MAJI SAFI
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava amezindua mradi wa maji Bukindo- Kagunguli (Tanki la Maji Kagunguli) wenye thamani ya Tshs. Bilioni 2.3 chini ya usimamizi wa wakala wa maji na usafi wa mazingira mjini na vijini (RUWASA).
Akizungumza na wananchi baada ya uzinduzi wa mradi huo leo Oktoba 8, 2024 uliojengwa na mkandarasi Otonde construction co ltd. Ndugu Mnzava amewataka wananchi kulinda miundombinu ya mradi huo ili uweze kuwasaidia kwa muda mrefu.
Aidha, kiongozi huyo ameiagiza jumuiya ya watumia maji kuhudumia wananchi kwa haki na usawa kwa kuzingatia bei ya maji inayoweza kuhimilika na mwananchi mwenye kila hali ya uchumi ili malengo ya kuipatia jamii maji safi na salama yatimie kwa wote.
"Naomba tuutunze mradi wetu na miundombinu yake ili iweze kutuhudumia kwa muda mrefu na tusimvumilie mtu atakayetaka kuhujumu lakini pia jumuia ya watumia maji siku zote tuhudumie jamii kwa usawa na haki kwenye bei kwa kuhakikisha inakua rafiki kwa wote."
Awali, Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Ukerewe Mhandisi Flowin Mkechi amesema mradi huo unahusisha matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 150,000 na kwamba wananchi elfu 23.2 kutoka kwenye vijiji vya Buzegwe, Nampise, Muhande na Buguza katika kata ya Kagunguli vimefikiwa na mradi huo.
Halikadhalika, kiongozi huyo wa mbio za mwenge mwaka huu amemkabidhi Bi. Khadija Nyankubi nyumba ya kisasa aliyojengewa na wadau kufuatia agizo la Mkuu wa Mkoa huo la kumpatia zawadi bibi huyo mzalendo aliyetoa eneo la ujenzi wa mradi huo bila kudai fidia.
Katika wakati mwingine, Mwenge wa Uhuru wilayani Ukerewe umezindua mabweni 3 ya kidato cha V na VI, madarasa 8 na matundu 33 ya vyoo vyenye thamani ya tshs. Milioni 694.2 katika shule ya sekondari Bukondo ambapo Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Emanuel Bomba ameishukuru Serikali kwa miundombinu hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.