Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amewaagiza Wakandarasi wanaojenga Miradi wa Maji ya Magu na Misungwi kukamilisha Ujenzi kwa wakati kwa mujibu wa Mkataba ili iweze kuwanufaisha wananchi zaidi ya elfu saba wanaoisubiria.
Ametoa agizo hilo (Jumanne hii Disemba 13, 2022) katika Hafla ya Kusaini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Lugeye - Kigangama unaotekelezwa na Mkandarasi Mponela Construction and Company Ltd kwa Bilioni 7.1 na Mradi wa Misungwi Lumeji- Magu chini ya Mkandarasi Lugaila Construction Ltd kwa Bilioni 1.8 dhidi ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa miezi 18.
"Hata kama leo umesifiwa kwa kutekeleza miradi vizuri, nakuomba pombe usiitie Maji, ili mie nawe tuendelee kuwa na mapenzi makubwa nataka unihakikishie kuwa ndani ya miezi 18 wananchi hawa wapate mradi wao ukiwa bora kabisa ili wanawake hawa waokoe muda wa kutafuta maji kwani maji safi na salama ni Afya kwa nyumba nzima." Amesisitiza, Mhe. Malima.
"Leo tunapokea mradi mkubwa wa maji hapa Magu ambao umewekewa saini ya kukamilika ndani ya miezi 18, yeyote atakayetuibia hata nondo huyo ni mhujumu uchumi na hatutamwacha tunamchukulia hatua kwani tupo macho kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati. " Mhe. Salum Kalli, Mkuu wa Wilaya ya Magu.
Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Clement Kivegalo amewataka Wakandarasi wa Miradi hiyo kuhakikisha wanajenga miradi hiyo kwa ukamilifu na uaminifu mkubwa na wahakikishe wanakamilisha ujenzi ndani ya muda ulioainishwa kwenye Mkataba kusiwe na kisingizio kwani Serikali ina adhma ya kuwapatia wananchi wake huduma ya Maji safi na salama.
"Ndani ya Mwaka huu wa fedha, tumesaini miradi yenye zaidi ya Shilingi Bilioni 800 iliyotapakaa nchi nzima na kwa Mkoa wa Mwanza pekee kuna miradi 43 iliyosainiwa chini yangu ambayo ina zaidi ya Shilingi Bilioni 125, hiyo ndio Serikali ya Rais Dkt. Samia inayolenga kumtua Mama ndoo kichwani." Amesisitiza Mkurugenzi.
Meneja wa RUWASA Mkoa, Mhandisi Godfrey Sanga amesema Miradi 43 inaendelea kutekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 125 Mkoani humo na kwamba mahitaji ya Maji yamekua makubwa na Serikali imeamua kuleta mradi mwingine utakaozalisha Lita Milioni 3.3 kwa siku tofauti na Lita Milioni 2.5 zilizokua zinazalishwa wilayani Magu.
"Kutokana na Sensa ya Mwaka 2022 Mkoa wa Mwanza una Watu Milioni 3.7, Magu ina watu laki 3 ambapo asilimia 77 wanapata huduma ya Maji Safi kupitia miradi Mbalimbali na kwa sasa tuna Miradi 8 inaendelea ambapo watu elfu 86 watafikiwa ifikipo Juni 2024 na kufanya upatikanaji kuwa asilimia 90." Mhandisi Sanga.
Mbunge wa Jimbo la Magu, Boniventura Kiswaga ameishukuru Serikali kwa kusikiliza wananchi na kuamua kuwaletea miradi mbalimbali katika kuwapatia huduma za kijamii na ametumia wasaa huo kushukuru uongozi wa Mkoa na Wilaya kwa kushirikiana kwenye ufuatiliaji wa miradi.
"Leo tumetia saini ya mradi mkubwa wa Maji wa Bilioni 7 na Mradi mwingine wa zaidi ya Bilioni 1 tumeambiwa umeenda kule Misungwi kwakweli siku za nyuma tulikua tunasikia tu sehemu zingine lakini sasa ni zamu yetu hapa Magu kupata neema hii, kwakweli tunamshukuru sana Mhe. Rais." Mwenyekiti wa Halmashauri ya Magu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.