FAMILIA NI NGUZO IMARA KATIKA KULINDA MAKUZI YA MTOTO: DKT. BITEKO
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mb.) amewataka Wanajamii kuweka nguvu katika kuimarisha familia kwa kuwa ndiyo nguzo imara katika kulinda na kusimamia makuzi bora ya mtoto.
Dkt. Biteko amesema hayo leo mei 24, 2025 mkoani Mwanza alipomwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufunga Maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya familia iliyoambatana na kongamano la Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto.
Dkt. Biteko amesema lengo la maadhimisho hayo kuunganishwa na malezi ya mtoto ni kuthamini mchango wa familia katika malezi na makuzi, Hivyo kwa namna yoyote kuiharibu familia ni sawa na kuharibu mustakhabali mzima wa mtoto.
“Ni kawaida kwa mzazi kuuliza kama mbuzi wake wameingia bandani lakini si mtoto wake anaendeleaje,”
Kadhalika Naibu Waziri Mkuu amezitaka familia na wanandoa kuacha utamaduni wa kuwashirikisha Watoto katika ugomvi na migogoro yao hatua aliyoitaja kuongeza hali ya uhasama baina ya wazazi na Watoto na kuwa sababu ya ongezeko la Watoto wa mitaani na mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Awali akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza tayari wamezindua mkakati wa kukabiliana na kutokomeza watoto wa mitaani, Aidha amesema kupitia futari maalumu aliyoiandaa na watoto wa mtaani alibaini kuwa wengi wao wametoka majumbani kutokana na sababu za migogoro ya familia.
Hivyo ameiasa jamii kuhakikisha wanazingatia matunzo ya watoto na kupunguza kuzaa nje ya ndoa kwani kwa kufanya hivyo kunapelekea pia kuibuka kwa changamoto za malezi na makuzi ya Mtoto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.