Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika usimamizi wa miradi ya maendeleo kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini, akisema kuwa jukumu hilo halipaswi kubebwa na watendaji wachache pekee.

Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo mchana wa leo Januari 30 wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Magu baada ya kubaini kuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nenge Mwl. Jonathan Paul alivuliwa cheo na kushushwa kuwa mwalimu wa kawaida kwa madai ya kushindwa kusimamia ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi Bugumangala.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa usimamizi wa ujenzi wa miradi ya maendeleo ni jukumu la pamoja linalohusisha watendaji mbalimbali, akiwemo Afisa Elimu, Mhandisi wa Halmashauri pamoja na Watendaji wa Kata na Kijiji, hivyo si sahihi kumuwajibisha Mwalimu Mkuu pekee huku watendaji wengine wakiachwa bila kuchukuliwa hatua.

Kutokana na hali hiyo, Mhe. Mtanda ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo Mwalimu Mkuu huyo alitendewa haki au la katika hatua iliyochukuliwa dhidi yake.

Aidha, Mkuu wa Mkoa ameagiza kuwa ujenzi wa Shule ya Msingi Bugumangala ukamilike ifikapo mwezi Machi mwaka huu, huku akisisitiza kuwa hatua stahiki zichukuliwe kwa watendaji wote watakaobainika kuwa walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Serikali imeleta fedha alafu nyie mnashindwa kuzisimamia tu kwa kujenga miradi, hii si sawa nataka wahusika wote mje mkeshe hapa usiku na mchana muhakikishe mradi huu unakamilika na si vinginevyo.”

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.