Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi mkoani humo kujiunga na huduma za bima ya afya kwa wote iliyozinduliwa kwa awamu ya kwanza na Waziri wa Afya Januari 26, 2026 ili kujihakikishia matibabu ya uhakika.

Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo tarehe 30 Januari, 2026 wakati akikagua ujenzi wa wodi ya wazazi katika kituo cha Afya cha Nyanguge kinachohudumia wananchi 22865 kutoka katika kata hiyo na kata jirani.

Mhe. Mtanda amesema ukamilifu wa wodi hiyo utasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hivyo ni lazima Mkurugenzi Mtendaji akamilishe kwa haraka ujenzi wa wodi hiyo kwa kuongeza pia fedha kiasi cha Tshs. Milioni 50 kwani serikali imeleta Milioni 200.

“Serikali imezindua mpango wa bima ya afya kwa wote, naomba liwepo dawati la huduma za bima ya afya ili wasihangaike na zile kero za wagonjwa kuomba msamaha au wakati wa kuwatoa ndugu zao waliofariki ziishe. “ Mkuu wa Mkoa.

Aidha, amewataka viongozi wa Mwanza kukamilisha taratibu za uanzishwaji wa eneo la uwekezaji ili lianze kazi kwani litainua uchumi wa wananchi wa mkoa wote wa Mwanza na akatoa wito kuepuka migogoro wa ardhi wakati wa utekelezaji wa mradi.

“Nataka niwaambie watu wa Magu, mkitaka mafanikio basi eneo la Viwanda la Matela B katika kijiji cha Matela ni lazima mulichagamkie kwa kukaa na wawekezaji kuona namna ya kufikia muafaka kwenye upimaji na uchukuaji wa maeneo kwa wanaanchi bila kusababisha migogoro.” Mhe. Mtanda.

Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amesema bima ya Afya kwa wote inatoa fursa ya kuunganishwa watu 6 kutoka kwenye Kaya kwa Tshs. 150,000 ambao watapata huduma kuanzia ngazi za zahanati hadi rufaa mkoa na hivi karibuni uandikishaji unaanza.

Ameongeza kuwa bima ya afya kwa wote inajumuisha huduma 372 kwa kiasi hicho tu cha fedha na inatoa fursa kwa matibabu ya upasuaji, madawa na hata huduma za dharula na kwamba inatoa fursa kwa wategemezi kuhudumiwa ndani ya kifurushi cha kaya ya watu sita tofauti na hapo awali.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.