Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025 Bw. Ismail Ali Ussi ameipongeza Halmashauri Manispaa ya Ilemela kwa kusimamia vema afua za lishe katika kuhakikisha wanafunzi wanapata vyakula vyenye virutubishi vinavyowasaidia kujenga afya bora wawapo shule.
Bwana Ussi ametoa pongezi hizo leo Agosti 26, 2025 wakati akikagua shughuli za usindikaji na uongezaji wa virutubishi kwenye ungalishe katika kiwanda cha Kipipa Limited kilichopo mtaa wa Sabasaba chenye thamani ya zaidi ya Tshs. Bilioni 1.2.
Amesema, viongozi wa Halmashuri hiyo wameonesha kwa vitendo kiu ya kuwalinda watoto na udumavu na utapiamlo kwani kwa kushirikiana na kiwanda hicho wanapeleka shuleni asilimia 18 ya bidhaa za vyakula zinazozalishwa kiwandani hapo.
“Ombi langu kwa wakulima na wafanya biashara kuunga mkono juhudi za serikali na kwa wanaomsimamia mwekezaji huyu kuchakata na kuzalisha bidhaa mbalimbali za nafaka kama mtama, mahindi na mhogo kwa kununua na kuwapatia watoto pamoja na wenye mahitaji maalum.” Amesema Bw. Ussi.
Aidha, amewapongeza wawekezaji hao kwa kubuni mradi mzuri ambao umezaa matunda ya uzalishaji wa tani 36.5 za nafaka na 5 za muhogo kwa mwezi na ametoa wito kwa Taasisi za kifedha kuendelea kuwatia moyo wawekezaji wa aina hiyo yenye tija ikiwemo Benki ya kilimo ambayo awali imewakopesha zaidi ya milioni 800.
Awali, Mwenge wa Uhuru umekagua mradi wa Kikundi cha Cross Over katika mtaa wa furahisha kabla ya uzindua malori 2 na kijiko kimoja mahsusi kwa ajili ya kuzolea taka kwenye Soko la kimataifa la Samaki Mwaloni pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari ya Ilemela.
Vilevile, mwenge wa uhuru umezindua ofisi ya kata Nyasaka pamoja na mradi wa jengo la mama na mtoto katika zahanati ya Nyakato kabla ya kuzindua huduma ya matumizi ya nishati safi katika shule ya sekondari Buswelu na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.