Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imezindua rasmi gari la mahakama inayotembea (mobile court) jijini Mwanza kwa lengo la kuisaidia usikilizwaji wa mashauri Mkoa ya Mwanza ambapo itaweka kambi maeneo la Buhongwa, Buswelu na Igoma.
Uzinduzi huo ulifanywa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Sam Rumanyika ambapo alisema matumizi ya mahakaa hiyo ni ya kisasa zaidi katika kusogeza huduma karibu na wananchi iliyopewa kauli mbiu ya “Niruhusu niseme mlangoni, mpe raha mteja mahakama ing’are”.
Jaji Rumanyika alisema gari hiyo ya kidijitali kwa mahakama itawapunguzia wananchi gharama na muda wa kutafuta haki mahakamani ambapo aliitaja jamii hasa wanawake kuchangamkia fursa hiyo.
“Kila ninapotafakari ujio wa aina hii ya mahakama katika kanda ya Mwanza naona ni kiwango cha bahati sana ukizingatia magari kama haya yapo mawili tu nchini, moja limebaki Dar es Salaam kwa ajili ya maeneo ya Kibamba, Bunju, Chanika na Buza, hivyo ni fursa ya kipekee kwetu.
“Inabidi tuchangamke kweli na tufikie mahali kama ikiwezekana yale mashauri yanayotokana na operesheni za uvuvi, uwindaji haramu yaletwe katika vituo vilivyopangwa na kutashughulikia haraka, kuna mashauri ambayo yataisha kwa siku moja na kutolewa hukumu.
“Tukumbuke kuwa katika takwimu zinaonyesha katika mahakama za mwanzo ndipo takribani asilimia 70 ya mashauri husajiliwa kila siku nchini nzima, hivyo siyo mbaya gari hili likaelekezwa kutoa huduma huko,”alisema Jaji Rumanyika.
Hata hivyo Mhe. Jaji Rumanyika aliwahimiza majaji na hakimu wa mahakama mbalimbali kanda ya Mwanza kuwahudumia kwa uharaka na kwa haki wananchi ili kuokoa muda wao na kwenda kujitafutia riziki na kujenga uchumi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Aliwataka majaji na mahakimu kutoa nakala ya hukumu ndani ya siku saba au papo hapo ingawa sheria zinaelekeza kutolewa ndani ya siku 21 ili kuondoa malalamiko yaliyopo ya ucheleweshaji na kusisitiza kuwa mtazamo wake ni kuona mahakama zinakuwa ‘fast track’.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella alisema ujio wa gari hilo linalotembea kutoa huduma za kimahakama linapaswa kutumiwa vema na watumishi wa sekta ya kisheria ili kuleta mabadiliko chanya.
Mhe.Mongella alisema hivi sasa hajapokea malalamiko mengi kutoka mahakama kuu juu ya kucheleweshwa kesi zao isipokuwa wananchi wengi wanalalamikia katika mahakama za mwanzo, hivyo aliomba kama ikiwezekana nguvu kubwa ielekezwe huko.
Ilielezwa kuwa gari hilo hadi kukamilika kwake limegharimu Sh milioni 470.8 huku likiwa na Televisheni, kamera zenye uwezo wa kurekodi ushahidi wote kwa picha na sauti, lifti kwa ajili ya watu wenye ulemavu na kipaza sauti kwa ajili ya kutangaza ratiba ya mahakama hiyo.
Itakumbukwa, Rais Dkt. John Magufuli alizindua gari hizo za mahakama inayotembea Februari 6, mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya sheria kwa ajili ya kutoa huduma ya usikilizwaji wa mashauri katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.