KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID KUONGEZA UELEWA WA HAKI NA MASUALA YA KISHERIA - WAZIRI NDUMBARO
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Damas Ndumbaro amesema uwepo wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia “Mama Samia Legal Aid Campaign” imesaidia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masuala ya haki, mifumo ya kisheria iliyopo, haki za binadamu na haki za makundi maalumu.
Mhe. Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo tarehe 18, Februari 2025 katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda wakati wa uzinduzi wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika katika viwanja vya Furahisha Wilayani Ilemela.
Aidha Mhe. Ndumbaro amesema kampeni hiyo imesaidia mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na masuala ya upatikanaji haki kwa ujumla.
“Kwa kuzingatia utelezaji wa kampeni hii, niwaombe wananchi watumie fursa hii, ili kumaliza migogoro hususani ya madai kwa njia za usuluhishi”.
Waziri huyo amesema pia Viongozi wa ngazi ya juu wana imani kubwa kwamba kupitia kampeni hiyo na elimu itakayotolewa, watendaji pamoja na wananchi watapata uelewa wa masuala ya kisheria, migogoro mingi iliyokuwepo katika ngazi za kijamii itatatuliwa na wananchi watapata huduma za msaada wa kisheria kwa urahisi na ufanisi.
“Hakika kundi la wananchi wanyonge, wanaoishi pembezoni na wasio na uwezo litakuwa limefikiwa kwa kiasi kikubwa na wengi sasa hawatapoteza muda mwingi katika kushughulikia changamoto zao za kisheria bali watajikita katika shughuli za maendeleo”. Ameongeza Waziri Ndumbaro.
Kabla ya kuhitimisha hotuba hiyo Mhe. Mtanda ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kupata huduma za msaada wa
kisheria zinazotolewa kwani masuala ya kisheria ni masuala mtambuka ambayo mwananchi anapaswa kuyafahamu na si kusubiri hadi upate changamoto.
“Kwetu sisi wana Mwanza ni upendeleo wa kipekee, msipoteze kabisa fursa hii adhimu”.
Tangu Kampeni hii ilipozinduliwa tarehe 22 Aprili, 2023 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) imetekelezwa katika Mikoa Kumi na saba (17) ya Tanzania Bara na leo tarehe 18 Februari, 2025 kampeni hii inazinduliwa katika Mkoa wa Mwanza na tarehe 19 Februari, 2025 Kampeni hii itazinduliwa katika Mkoa wa Lindi. hali hii inafanya jumla ya mikoa 19 kufikiwa na kampeni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.