Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi, akisisitiza kuwa kipimo cha utendaji ni usimamizi bora wa miradi.

Agizo hilo limetolewa tarehe 19 Januari 2026 katika kijiji cha Mwasonge Wilayani Misungwi wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa madarasa 3 na matundu 6 ya vyoo katika Shule ya Msingi Mtakatifu Benjamin uliokwama.

Mhe. Mtanda amesema ni utovu wa nidhamu kuchelewesha miradi ilhali serikali imetoa fedha, akibainisha kushindwa kukamilika kwa miradi ya BOOST licha ya Halmashauri kupokea zaidi ya Sh bilioni 1.14 tangu Juni 2025.

Amesikitishwa na uzembe uliochelewesha lengo la serikali la kupunguza msongamano wa wanafunzi, na kumtaka Mkurugenzi kukamilisha miradi 8 ya elimu ndani ya siku 10 na kuchukua hatua dhidi ya wasambazaji wazembe.

“Mkurugenzi hakikisha unachukua hatua za haraka za kisheria na kiutawala dhidi ya msambazaji wa vifaa aliyeshindwa kutimiza masharti ya mkataba katika ujenzi wa Shule hii na uzembe wa aina hiyo hautavumiliwa”.

Pia ameeleza kuwa uzembe huo umechelewesha ujenzi wa shule mpya ya Kigara inayogharimu Sh milioni 342, ambayo bado ipo hatua za awali licha ya fedha kupokelewa miezi sita iliyopita.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.