Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amepokea madaktari bingwa na bobezi 58 wa Mama Samia wa awamu ya nne kutoka katika kada sita ambao wamekuja kuweka kambi za matibabu katika Hospitali za Wilaya na Halmashauri 8 za Mkoa huo.
Madaktari hao wataweka kambi Mkoani Mwanza kuanzia tarehe 20 hadi 24 Oktoba 2025 wakitarajiwa kutoa huduma za Ubingwa katika maeneo ya magonjwa ya ndani, wanawake na ukunga, upasuaji, ubobezi kwa watoto wachanga, ubingwa katika huduma za kinywa na meno, usingizi na ganzi, pamoja na huduma za ubingwa na ubobezi katika uuguzi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kambi hiyo Bw. Balandya amesema ujio wa madaktari hao bingwa ni wa faida kwa watumishi wa idara ya afya pamoja na wananchi kwani utasaidia katika kutoa elimu, mafunzo na huduma.
“Naamini kwamba ujio wenu katika Mkoa wa Mwanza utasaidia kukuza ujuzi wa hawa wenzetu waliopo katika Mkoa huu ili waweze kuondokana au kupunguza changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi”. Amesema Bw. Balandya.
Aidha, amewahakikishia wataalamu hao kupata ushirikiano kutoka ngazi ya Mkoa na Halmashauri kwa kipindi chote ambacho watakua wameweka kambi Mkoani humo, huku akiwakaribisha wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupatiwa matibabu.
Vilevile, Katibu Tawala ametumia wasaa huo kuishukuru serikali kwa kuwaletea wataalamu hao huku akibainisha kuwa mara zote imekua ikihakikisha inaboresha huduma na miundombinu mkoani humo na akazitaja Bilioni 63 zilizotolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu na vifaa tiba kwa kipindi cha miaka 4.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amewasisitiza madaktari hao bingwa kwenda kubadilishana ujuzi na madaktari ambao watawakuta katika hospitali za Wilaya.
Msimamizi wa timu hiyo kutoka Wizara ya Afya Bi. Fidea Obimbo amesema lengo kubwa la kambi ya madaktari bingwa na bobezi kufika Mkoani Mwanza ni kuwafikia wananchi kwa huduma tofauti ambazo zilikua ni ngumu kwao kuwafikia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.