Makarani wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoani Mwanza leo Agosti 11, 2022 wamefanya mafunzo kwa vitendo kwaajiri ya kutambua mipaka na kuhoji wanakaya kwa majaribio katika maeneo mbalimbali huku wakitumia Madodoso yaliyopo kwenye Vishikwambi.
Mkufunzi wa Mafunzo ya Sensa ngazi ya Mkoa kutoka kituo cha Maliasili, Sambona Peres amesema katika kituo chao wamewaandaa Makarani kuwa mabalozi kwa wananch kwa kuelimisha jamii juu ya zoezi hilo ili siku ya Sensa zipatikane takwimu sahihi.
Wakizungumza katika nyakati tofauti Makarani hao wamesema wapo tayari kwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwani wamepatiwa mafunzo bora ya kuwawezesha kufanikisha zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika jumanne ya Agosti 23, 2022 nchini.
Innocent Mijaya, Mwenyekiti wa Mafunzi Butimba amesema zoezi la dodoso la mipaka na sensa kwa mafunzo ni la siku moja na baadae watarudi tena kwa zoezi la kudodosa dodoso la majengo na kwamba kwa kutumia vishikwambi karani anaonekana amepita kwenye mipaka gani na nini amehoji.
"Kwa takribani siku 12 tumepata mafunzo ya nadharia darasani na sasa tupo katika mafunzo ya uwandani ambapo moja ya kazi ya karani ni kutambua mipaka kabla ya zoezi la kudodosa wanakaya waliopo ndani ya mipaka yake, na ndiyo kazi leo tunayofanya". Amesema Innocent.
Naye, Karani Joyce Ndomaa amejinasibu kuwa kwa kupitia mafunzo hayo ya vitendo wamekagua mipaka ya eneo la ziwa namba 2 Butimna na kwamba zoezi hilo la vitendo limewasaidia kuelewa zaidi kufuatana na mafunzo waliopewa darasani.
"Kwa sasa watu wanashangaa hivi tulivyoshika ni vitu gani, nasi tunaanza kuwaelimisha kuwa vifaa hivi ni vya kazi gani na tunawashukuru Wenyeviti wa mitaa na watendaji ambao wanatusaidia sana kufanikisha zoezi hili." Amesema Nyanda Patrick ambaye ni Karani kutoka darasa la Butimba.
Karani Mary Nyirenda ametoa rai kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa zoezi la Sensa ya watu na makazi huku akibainisha kuwa kwenye eneo la Kawekamo wamekutana na changamoto kama za wanakaya kutokubali kuzungumza, kukataa kuhojiwa na kupelekea kupata taarifa zisizo sahihi kwa baadhi ya kaya hali ambayo inasababishwa na kutowakuta wakuu wa kaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.