Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka watumishi wa sekta ya afya mkoani humo kutumia kikamilifu Mfumo wa Kielektroniki wa GoT-HOMIS ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuboresha usimamizi wa dawa na huduma kwa wagonjwa.

Ametoa wito huo leo Januari 19, 2025 alipokuwa akikagua utoaji wa huduma na maendeleo ya ujenzi katika Kituo cha Afya Usagara Wilaya ya Misungwi ambapo amepongeza ufanisi wa mfumo huo uliosaidia kuongeza mapato kutoka Shilingi 200,000 hadi Shilingi Milioni 8 kwa mwezi.

Mhe. Mtanda amesema awali Mkoa ulikuwa nyuma katika ukusanyaji wa mapato kupitia sekta ya afya lakini matumizi ya GoT-HOMIS yameongeza mapato na kurahisisha upatikanaji wa takwimu za wagonjwa, dawa na mapato.

Aidha amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi aliyesababisha migogoro katika kituo hicho na kudhoofisha utoaji wa huduma.

“Tunataka watumishi na viongozi wanaounganisha watu na sio wanaowagawa watu, watumishi wasiofanya kazi kwa weledi hatuwataki.” Ameongeza Mhe. Mtanda wakati akisisitiza masuala ya kinidhamu ikiwemo kuwahi kazini.

Kituo cha Afya Usagara kinahudumia wananchi 3,348 na kinaendelea na uboreshaji wa miundombinu ikiwemo OPD, maabara, kichomea taka, wodi ya wazazi na jengo la upasuaji kwa ufadhili wa Serikali na tozo za miamala ya simu.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.