MHANDISI LUHEMEJA: USAFI WA MAZINGIRA SASA NI LAZIMA KUTOKOMEZA MAGUGU MAJI
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa maagizo ya kufanyika kampeni maalum ya usafi wa mazingira kwenye mialo yote inayozinguka ziwa Victoria ili kutokomeza ukuaji wa magugu maji ambayo yamezidi kushamiri ziwani humo.
Akitoa maelekezo hayo mapema leo asubuhi Machi 10, 2025 kabla ya kuanza zoezi la kukagua hali halisi ya magugu maji hayo eneo la Kigongo Wilayani Misungwi, Luhemeja amebainisha kampeni hiyo ya usafi sasa siyo ya hiari bali ya lazima na kuwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuitikia wito huo ili kuepukana na hasara za kuwepo magugu maji hayo ziwani.
"Ndugu zangu hali halisi tunaiona mbele yetu siyo nzuri, hali ya usafiri inazidi kuwa ngumu na ukuaji wa viumbe maji upo hatarini, ni lazima hatua za haraka zianze tukianzia na azimio la usafi”. Amesisitiza Mhandisi Luhemeja.
Amesema wamelazimika kuja na Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maji, na Viongozi wengine waandamizi kutoka Tamisemi na Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka Kanda ya ziwa, lengo ni kukutana na kutoa jawaba la haraka kulinusuru ziwa Victoria na janga hilo.
Aidha Katibu Mkuu huyo mara baada ya kupata taarifa fupi kutoka kwa Meneja wa Kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Bw. Joram Kayombo kwamba nchi ya Uganda wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokomeza magugu maji, ameagiza wataalamu kutoka nchini kwenda huko ili kupata uzoefu wa kitaaluma ili kuja kusaidia kukabiliana na hali hiyo.
Awali akiwakaribisha Ofisini kwake viongozi hao waandamizi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema magugu maji yamekuwa tishio katika kukuza uchumi wa buluu kutokana na uwepo wake kunashusha mazalia ya viumbe maji, shida ya usafiri na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba nao kuwa mgumu.
"Nina imani na timu hii iliyochanganyika na wataalamu tofauti na masuala ya mazingira kuja na jawabu chanya ili kuendelea kulipa uhai ziwa Victoria”. Mhe. Mtanda.
Viongozi hao waandamizi kutoka Wizara mbalimbali siku ya kesho watakutana kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa le ngo la kutoa maazimio kukabiliana na janga hilo la magugu maji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.