*Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara,Rai ya ujenzi wa Taifa imara yatolewa Mwanza.
Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara yamefanyika leo nchini huku Rai ya kuthamini amani na umoja na kulijenga Taifa kiuchumi ikihimizwa kwa Watanzania.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg.Balandya Elikana akizungumza katika maadhimisho hayo Wilayani Magu amesema hakutakuwa na maana kama tunafanya maadhimisho haya huku amani miongoni mwa Watanzania ikiwa hakuna ni dhahiri Taifa haliwezi kuwa na Maendeleo yoyote.
Amesema Nchi yetu imebarikiwa kuwa na amani na umoja ulioasisiwa na Viongozi wetu Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere na Abeid Karume na tumeendelea kuona maendeleo ndani ya Taifa letu tangu Uhuru hadi sasa.
"Wakati wa miaka ya Uhuru Mkoa wa Mwanza ulikuwa na shule za Sekondari 5 lakini sasa tunazo 317,Hospitali zilikuwa 3 za Wilaya lakini sasa tunazo 26 wakati huduma ya maji ilikuwa inawafikia watu kwa asilimia 19 lakini sasa ni asilimia 60 Wananchi wanapata rasilimali hiyo" amesema Mtendaji huyo Mkuu wa Mkoa.
Amewakumbusha wananchi kuendelea kuwaenzi kwa vitendo Viongozi wetu waliopigania Maendeleo ya Taifa hili kwa kufanya kazi kwa bidii,ubunifu na kutanguliza uzalendo.
"Tunaona kasi ya maendeleo inayofanywa na Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan,kila mwananchi ana kila sababu ya kuunga mkono jitihada hizi ambazo ni kwa faida yetu na vizazi vijavyo"amesisitiza Ndg.Balandya
Awali akitoa salamu za Wilaya ya Magu Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Salum Kalli amesema Miradi mingi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya afya na shule imetokana na uimara wa Serikali ya awamu ya Sita ambayo imeonesha kwa vitendo dhamira ya kumletea maendeleo mwananchi.
Maadhimisho hayo yaliyokwenda pamoja na Mdhahalo uliolenga tumetoka wapi,tulipo sasa na tunakwenda wapi tangu kupata Uhuru wa Tanzania Bara,"Tujifunze kutanguliza uzalendo,kuepuka tamaa na kuridhika na kipato halali,kwa kufanya hivyo tutaepuka rushwa na kujenga Taifa lenye weledi"Mchungaji Dkt.Jacob Mutash.
"Tujenge utamaduni wa kuwapenda Viongozi wetu,tuwakosoe kwa busara na kuepukana na siasa za kusigana na chuki tukizingatia haya tutazidi kuwaenzi kwa vitendo waasisi wetu ambao miongozo yao imezidi kutuimarisha siku hadi siku"Padri John Kasembo mwalimu na mshauri wa viongozi.
Tanzania Bara imepata Uhuru wake Disemba 9 1961 kutoka kwa mkoloni Muingereza,huku kila mwaka yakifanyika maadhimisho hayo kwa kushiriki shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.