Wizara ya Afya imeridhishwa na utayari kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwemo Mwanza kuhusiana na ugonjwa wa Ebola ambao umetokea huko nchini Uganda na kuhimiza elimu kwa umma itolewe ili Wananchi wapate ufahamu wa kutosha kuhusiana na ugonjwa huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi akizungumza leo na vyombo vya habari kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema amefanya ziara Mikoa ya Kagera na Mwanza kujionea hatua zilizochukuliwa kwa tahadhari ya ugonjwa huo na kuridhika huku akitaka Wataalamu wote wa afya kujikita kutoa elimu kuanzia mtaani na kwenye vyombo vya Habari.
"Niwafahamishe Wananchi nchi yetu ipo salama hakuna mgonjwa yoyote aliyegundulika hadi sasa lakini tusibweteke na badala yake tuelimike vyema na kujenga utamaduni wa kunawa mikono mara kwa mara kwani ugonjwa wa Ebola unaambukizwa kwa njia ya vimelea vya maji na damu" amesema Katibu Mkuu.
Mtendaji huyo Mkuu kutoka Wizara ya Afya amewataka Wataalamu wa Afya waliopo kwenye Viwanja vya Ndege na Bandari kuongeza umakini na usahihi wa taarifa za wanaoingia na kutoka kupitia mifumo ya kisasa ili kuudhibiti ugonjwa huo.
Kwa upande wake kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw Daniel Machunda akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoani humo Balandya Elikana, amemuhakikishia Profesa Makubi kuwa Mkoa wa Mwanza umeyapokea na kuyafanyia kazi maelekezo yote kutoka Wizarani ili Wananchi waendelee kubaki salama.
"Mara baada ya kutokea visa vya ugonjwa wa Ebola nchini Uganda Mwanza tulianza kuchukua tahadhari mara moja kwa kutenga vituo vya kuwapokea wagongwa watakaogundulika na kuhakikisha vifaa vyote muhimu vipo tayari" Kaimu Katibu Tawala.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt Thomas Rutachunzibwa amebainisha kuwa kwa kutambua hatari ya ugonjwa wa Ebola kila Halmashauri imetenga Vituo vya kuwapokea wagonjwa watakaobainika.
"Hapa Mwanza mjini tuna vituo vitatu vya Buswelu, Mkuyuni pamoja na Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Sekou Toure pia Hospitali ya Kanda ya Bugando ipo tayari endapo itatokea visa vya ugonjwa huo" amesema Mganga Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Dkt. Rutachunzibwa amesema wametoa elimu ya kutosha kwa Wataalamu wote wa afya ili kuhakikisha wanakuwa salama endapo itatokea hali ya kumhudumia mgonjwa wa Ebola.
Miongoni mwa dalili za ugonjwa wa Ebola ni homa kali, mwili kuchoka bila sababu, kutokwa na damu kwenye matundu yote ya mwili, kuharisha na kupoteza fahamu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.