MWANZA WAONGOZA MATOKEO YA MTIHANI WA UTAMILIFU KANDA YA ZIWA
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emily Kasagara leo Agosti 20, 2024 ametangaza matokeo ya utamilifu kidato cha nne kwa mikoa ya kanda ya ziwa ya Geita, Simiyu, Kagera, Mara na Mwanza yenye ufaulu wa GPA 3.9 kwa asilimia 84.48 (Daraja la kwanza hadi la nne).
Akitangaza matokeo hayo Kasagara amefafanua kuwa ufaulu wenye tija daraja I- III ni asilimia 26.48 GPA ya 2.4 na kwamba ufaulu umejikita katika daraja la 4 kwa asilimia 13.01 huku daraja sifuri ni asilimia 9.02 na akawataka walimu kuwajibika ili kupandisha ufaulu hususani madaraja 1, 2 na 3.
"Mkoa wa Mwanza umeongoza kwa GPA ya 3.72 kwa asilimia ya ufaulu wa asilimia 86.13 ikifuatiwa na Mkoa wa Simiyu na tunazipongeza halmashauri za Manispaa ya Ilemela, Jili la Mwanza na Bukombe DC kwa kufanya vizuri." Amesema Kasagara.
Vilevile, ndugu Kasagara ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuamini kuwa elimu ndio nyenzo ya kuaminika inayowezesha kila mtu kuyakabili mazingira yake kwa usahihi kwa kujipatia maendeleo endelevu kwa kutoa fedha za elimu bila ada kwa shule za msingi na sekondari jambo linalochangia kukuza ufaulu.
"Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu kwa kukarabati shule kongwe na kujenga shule mpya na kuongeza miundombinu kama madarasa, mabweni, maabara na vyoo." Ameongeza Kasagara.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza Martin Nkwabi amefafanua kuwa malengo ya mitihani hiyo siyo kujikita tu kwenye kuona mwanafunzi amefeli au amefaulu bali ni kujipima kwenye ufundishaji wa walimu ili kurekebisha kasoro kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mitihani wa mwisho ya kumaliza elimu ya sekondari.
Aidha, amewataka walimu kuwajibika kuhakikisha wanapandisha matokeo kwa watoto kwenye madaraja ya kwanza hadi la tatu kama walivyowekeana malengo hususani mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha wanafuta daraja ziro na kupunguza daraja la nne kwa wanafunzi.
"Nataka kila mkuu wa shule afanye tathmini na akatafute sababu ya matokeo aliyoyapata na kuhakikisha anarekebisha kasoro hizo ili tupate ufaulu wa zaidi ya asilimia 60 kwa wanafunzi wetu ili kuhakikisha tunafuta daraja ziro na daraja la nne." Afisa Elimu Mkoa.
Matokeo hayo ya mtihani uliofanyika Julai mwaka huu yanapatikana kupitia https://sras.ac.tz ambapo kila mmoja anaweza kuona na yamepangwa kwa mpangilio wa mikoa, halmashauri na shule.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.