Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Dtk. Philis Mishack Nyimbi ameahidi kutoa millioni 200 kwa wafanya biashara wadogo wadogo ili waweze kujiongezea mitaji na kuendelea kuchangia uchumi wa nchi.
Mhe.Dkt.Nyimbi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika soko kuu la Mwanza pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo aliowakuta katika eneo hilo.
"Naahidi kutoa cheki ya millioni 200 kwa wafanya biashara wadogo wadogo na wajasiliamali ambapo fedha hiyo inatoka Halmashauri ya jiji la Mwanza na itagawiwa kwa vikundi mbalimbali vya kina mama, vijana na walemavu hivyo itasaidia kuleta maendeleo katika jamii," alisema Mhe. Dkt.Nyimbi.
Hata hivyo Mhe.Dkt Nyimbi aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa na Wilaya kama Sehemu ya kujitambulisha kwa wananchi na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naye Mhe. Mongella katika ziara hiyo amesisitiza swala la usafi,usalama pamoja na kufanya kazi kwa juhudi kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuondoa maisha magumu kwa wananchi na kuongeza kipato cha familia na nchi kwa ujumla.
"Nahitaji ushirikiano kutoka kwenu zaidi, pia nawapongeza wamachinga kwa kuleta amani na utulivu kwenye jiji letu la Mwanza kwa kupunguza uhalifu kwani mnatupa ushirikiano mkubwa, hata hivyo nahitaji zoezi la usafi la kila Jumamosi liendelee ili kuepuka ugonjwa wa kipindupindu.
Aidha ameongeza kuwa kwa kuendeleza kauli ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kila mtu ajitume kwa nafasi yake na kufanya kazi kwa bidii kwani Mhe.Rais anasema "Hapa kazi tu."
Mhe. Mongella aliwasisitizia swala la kulipa kodi kwa kila mfanya biashara hata kama ni kiasi kidogo kwani kwa kufanya hivyo wanachangia maendeleo ya nchi.
Mhe. Mongella alitembelea pia shule ya Nyakato B na kuongea na wanafunzi ambapo amewasisitiza kusoma kwa bidii ili kuweza kufikia malengo yao na alitoa zawadi ya fedha kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na la tatu waliojibu maswali yake kwa ufasaha ili kununulia madaftari na kalamu.
Hata hivyo kamati ilimalizia ziara hiyo kwa kutembelea Zahanati ya Isebanda, Wasambazaji wa dawa za kilimo na mifugo( Twiga Chemical Industries), pamoja na Shule ya Nyakato B.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.