Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana akiwa ameongozana na wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa pamoja na Wakuu wa Idara kutoka Sekretarieti ya Mkoa amefanya ziara wilayani Sengerema kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akiongea katika mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya sekondari katika kijiji cha Isungang’holo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Sengerema kuhakikisha huduma za msingi kama Umeme shuleni hapo pamoja na kuweka uzio na kupanda miti ili kutunza mazingira.
Aidha, ameiagiza kamati ya ujenzi wa shule ya msingi Nyanango (Buchosa) pamoja na Isungang’holo kusimamia unadhifu wa mazingira ya shule hiyo kwani serikali imewekeza zaidi ya Tsh. Milioni 580 ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora hivyo hawana budi kuenzi juhudi hizo.
Akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Sima, Katibu Tawala amewahakikisha wakazi hao huduma ya maji safi siku za usoni kutokana na mradi mkubwa wa maji unaojengwa kwa zaidi ya Tshs. Bilioni 3 pamoja na changamoto kadhaa zilizochelewesha mradi huo kutokamilika mwaka 2023 sasa zimeshashughulikiwa.
Halikadhalika, ameiagiza Halmashauri hiyo kukamilisha ujenzi wa madarasa yanayojengwa katika shule ya msingi Nyasenga Nyampande pamoja na kuhakikisha wanaweka mitaro ya maji katika ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka CCM hadi katikati ya mji wa Sengerema.
Akikagua huduma za Afya wilayani humo, Bw. Balandya ameitaka Halmashauri ya Sengerema kukamilisha nyumba ya familia mbili inayojengwa katika Zahanati ya Butunga pamoja na Buchosa kuharakisha ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Nyabutanga ili wananchi wapate huduma za afya jirani na makazi.
Vilevile, Katibu Tawala amewaagiza RUWASA kusanifu na kupanua upya mradi na kuhakikisha wanapeleka huduma ya maji safi kwenye vitongoji vya Itabagumba, Mbugani na Bulyaheke A na B kupitia mradi wa zaidi ya Tshs. Bilioni 3 unaotekelezwa katika kijiji cha Kazunzu kabla ya kupeleka maji hayo katika maeneo ya mbali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.