Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amemuagiza Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na Idara ya Mipango kuhakikisha wanafanya Marekebisho ya Mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuhakikisha Kampuni ya Misungwi Company Ltd inamilikiwa na Halmashauri kwa asilimia 100.
Akizungumza kwa niaba yake leo tarehe 21 Juni, 2023 Katibu Tawala Mkoa Ndugu Balandya Elikana wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani Maalum la Kujadili Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa fedha 2021/22 amesema haiwezekani Kampuni ya Serikali ikaanzishwa na kuendeshwa kwa kukiuka taratibu za umiliki wa Makampuni ikiwemo Mkurugeni wa Halmashauri kuwa Mbia binafsi.
Vilevile, ameiagiza TAKUKURU ndani ya siku 30 kufanya uchunguzi ili kubaini uendeshwaji wa Kampuni hiyo iliyoanzishwa kwa hati ya Usajili Na 140457876 Novemba 21, 2019 ikiwa na Mali za TZS 35,547,983 na fedha Taslimu TZS 24,547,983 na thamani ya Mashine TZS 11,000,000 huku ikiwa na udhaifu kwenye Muundo na Usimamizi na kukosekana kwa gawio la moja kwa moja kwa Halmashauri hiyo.
Aidha, Elikana ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata Hati safi na amewataka kuwa na Mwenendo wa kushughulikia Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu kwa haraka ili kujihakikishia wanaendelea kupata Hati safi na kwamba hilo linawezekana endapo watafuata taratibu na Kanuni za Mapato na matumizi ya Fedha za umma.
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi, Mweke Hazina wa Halmashauri hiyo Ngugu Joseph Mazito amesema pamoja na kupata Hati Safi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali katika mwaka 2021/22 alitoa hoja 16 ambazo zilitakiwa kujibiwa na kuwasilisha majibu kwa ajili ya uhakiki
"Hadi kufikia tarehe ya kikao hiki majibu ya hoja hizo yaliwasilishwa na kuhakikiwa na hoja zilizotekelezwa na kufungwa ni 12 sawa na asilimia 75 huku hoja zinazoendelea kutekelezwa zikiwa ni 4 sawa na Asilimia 25 ambapo jitihada zinaendendelea kuhakikisha zinajibiwa." ameeleza Mwekahazina.
Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Nje Mkoa wa Mwanza, Waziri Shaban ameipogeza Halmashauri ya wilaya ya Misungwi kwa kupata Hati safi na akabainisha kuwa wamekua na mwenendo wa kupata Hati Safi kwa zaidi ya miaka 3 mfululizo na ametoa wito kwa watendaji kuheshimu taratibu za fedha.
"Tunawapongeza Halmashauri ya wilaya ya Misungwi kwani kwa Mwaka wa fedha 2021/22 Halmashauri hiyo ilikaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na imepata Hati safi huku wakiwa na Agizo moja tu la LAAC ambalo hawajalitekeleza na kuonesha juhudi za kuitekeleza" amesema Ndugu Waziri Shaban.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.