RC MAKALLA APIGA KAMBI YA SIKU TATU VISIWA VYA UKEREWE
*Amshukuru Rais Samia kwa kutoa Bilioni 34 Kujenga Vivuko Vipya kuboresha Usafiri visiwani*
*Amshukuru pia kwa Kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwenye Wilaya hiyo iliyo kisiwani*
*Makalla afafanua kuwa zaidi ya Bilioni 22 zitatumika kuboresha huduma za Maji kisiwani Ukerewe chini ya RUWASA*
*Abainisha kuwa Rais Samia atoa Bilioni 130 kupeleka Umeme Ukerewe*
*Awaagiza Halmashauri ya Ukerewe kutoa kipaumbele kwa wazabuni wazawa*
Leo jumanne Novemba 21, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amefika Kisiwani Ukerewe kwa ziara ya Siku tatu ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na ukaguzi wa Miradi ya maendeleo ambapo anatarajia kufika kwenye baadhi ya Visiwa kikiwemo Ukara.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo, Mhe. Makalla amempongeza Rais Samia kwa kuboresha huduma za usafiri wa Majini kwa kutoa Bilioni 34 kujenga vivuko vipya 10 mkoani huko kikiwemo cha Rugezi- Kisorya wilayani Ukerewe ambacho ifikapo mwezi Aprili 2024 kitaanza kutumika na kusaidia kuimarisha usalama wa abiria.
Amesema kuwa Rais Samia amekua mlezi bora kwa kujali wananchi wake kwani anahakikisha anaboresha maisha ya kila mtanzania kwa kupeleka huduma bora kila kona na ndio maana wananchi hususani wa visiwani kama Ukerewe na Visiwa vingine 38 vinavyozunguka wilaya hiyo ameamua kuwapelekea vivuko vipya ili wawe salama wakati wote wanaposafiri.
Vilevile, Mhe. Makalla amesema wananchi zaidi ya 887,000 wa Wilaya hiyo siku za karibuni watanufaika na huduma za Kibingwa za afya kutokana na kujengewa hospitali ya Rufaa yenye hadhi ya Mkoa na kwamba tayari zaidi ya shilingi Bilioni nne zimepelekwa na ujenzi umeanza.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amendelea kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kudhamiria kumaliza tatizo la nishati ya Umeme na ameshatoa Bilioni 130 kwa ajili ya Ujenzi wa mradi mkubwa na kwamba mkandarasi ameshapatikana ambaye atajenga miundombinu kwa kilomita 98 pamoja na kituo cha kupoza umeme.
"Rais Samia anawapenda wananchi wa Ukerewe, jiandaeni na umeme wa uhakika na mkandarasi ameshapatikana na siku za karibuni ataanza kazi na kambi yake itakua kwenye kijiji cha Malegea", amefafanua Mhe. Makalla wakati akielezea mradi utakaohusisha njia ya usafirishaji yenye umbali wa Kilomita 98 pamoja na kituo cha Kupoza umeme.
Halikadhalika, CPA Makalla amebainisha kuwa wananchi wa Nansio, Ukara, Bukindo, Irugwa, Sizu na Gana wanajengewa miradi mikubwa ya maji ambayo ukamilifu wake utawapatia maji aafi na salama na kuimarisha afya na kwamba itaondoa adha hiyo kwa wananchi.
Akijibu kero zilizowasilishwa na Ndugu Leberatus Mulebele Mhe. Makalla amewataka Halmashauri ya Ukerewe kutoa zabuni kwa wafanyabiashara wazawa ili kuwainua kiuchumi na kuhakikisha wanatoa muongozo wa uchangiaji kwa wananchi kwenye huduma za usafiri wa gari la wagonjwa na inapotokea rufaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.