RC MAKALLA AWATAKA WADAU WA ELIMU MWANZA KUBORESHA ELIMU, KUAINISHA MIPAKA YA SHULE MAPEMA
*Asema kipaumbele chake ni kuboresha elimu, kuongeza ufaulu*
*Wazazi waelimishwe kuhusu umuhimu wa kuchangia chakula kwa wanafunzi*
*Amshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha nyingi kwenye miradi ya elimu*
*Wakuu wa Wilaya awataka kusimamia mikutano ya kuboresha elimu kwenye maeneo yao*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla amewataka wadau wa elimu Mkoani humo kusimamia vyema
maendeleo ya elimu na kuepuka migogoro ya ardhi kwa kuainisha mipaka yao mapema kwa kuweka beacon.
Akizungumza leo na wadau wa elimu kutoka Wilaya zote za Mkoa huo kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari Loreto, Mkuu huyo wa Mkoa amesema uboreshwaji wa elimu utakuwa na mafanikio endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa weledi kuanzia ngazi ya Maafisa elimu kata.
"Leo tupo hapa yakiwa ni maelekezo yangu ya kutaka tukutane na tupeane mikakati kamambe ya namna ya kuboresha elimu Mkoani kwetu,bado zipo changamoto za hapa na pale ambazo tukienda kuzisimamia vyema tutafika katika malengo yetu",CPA Amos Makalla.
Amesema Serikali ya Rais Samia imeleta fedha nyingi kuboreha Sekta ya elimu Mkoani Mwanza ikiwemo shule ya wasichana Magu ya kidato cha tano na sita iliyogjarimu Shs bilioni 3,wajibu wa wadau hao ni kuhakikisha wanajituma ili kuleta matokeo chanya
Amewaagiza wadau hao kutoa nafasi ya kutosha ya kuwaelimisha wazazi na walezi wa kuona umuhimu wa kuchangia chakula shuleni hali ambayo italeta tija kwa wanafunzi ya kuwa na usikivu mzuri wa masomo na hatimaye kufanya vyema katika masomo yao.
"Hapa nawaomba tuelewane vizuri tutangulize busara katika kuwaelimisha wazazi,epukeni kutumia aina yoyote ya nguvu, vitisho au kumrudisha mtoto nyumbani,wakuu wa Wilaya muwe mstari wa mbele kusimamia mikutano hii ili kuwepo na upana mzuri wa uelewa katika jambo hili",amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Kuhusu suala la utoro shuleni,Makalla amewataka wakuu wa Shule kufanya ufuatiliaji kwani Serikali imesha weka mazingira mazuri ya watoto kusoma kwa kuondoa malipo ya ada.
Ameongeza kuwa wapo baadhi ya wazazi wanaowatumikisha watoto wao kazi badala ya kuwapeleka shule,mabinti kuozwa mapema na watoto wa kiume kukimbilia kwenye shughuli sehemu za machimbo ya madini,yote hayo yanapaswa kufanyiwa kazi kuanzia kwa Maafisa elimu kata kwa lengo la kuboresha sekta ya elimu.
Awali akitoa utangulizi wa kikao hicho,Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu,Ndg.Daniel Machunda aliyemuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa, amesema malengo ya kikao hicho ni kupata maelekezo yake namna ya kuboresha elimu, taarifa za maendeleo ya elimu na kupokea maoni ya wadau mikakati ya kufikia malengo.
Kikao hicho kimewajumuisha wadau wa elimu 670 wakiwemo,wakuu wa Shule za Sekondari Maafisa elimu kata ,Maafisa elimu wa Halmashauri,Wakurugenzi, na baadhi ya wabunge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.