RC MAKALLA AZIASA NG'O KULINDA MAADILI YA KITANZANIA
Atoa wito kufanya kazi kizalendo na kwa uwazi
Ayaagiza mashirika hayo kufuata sheria za nchi na kuwa tayari kukaguliwa
Amewasihi kufikisha huduma kwenye maeneo ya vijijini
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi kwa kufuata sheria za nchi na kulinda mila, tamaduni na desturi ili kujenga jamii yenye maadili.
Ametoa wito huo leo wakati wa kilele cha Mkutano/Jukwaa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Mwanza lililofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
CPA Makalla amesema mashirika yasiyo ya Serikali ni nguzo muhimu katika kujenga uchumi wa nchi lakini wanapaswa kuenenda kwa kufanya shughuli kwa mujibu wa usajili wa taasisi zao.
"Mashirika yasiyo ya Kiserikali ni wadau muhimu wa maendeleo nchini na ndio maana hata kwenye Bajeti ya Serikali utasikia eneo la wafadhili nami nawapa ahadi ya ushirikiano wakati wote maana hata kwenye mabanda nimeona mnajihusisha na huduma muhimu za kijamii kama Elimu na Afya."Makalla.
Aidha, amewaahidi kupokea ushauri wa aina yoyote kutoka kwenye mashirika hayo huku akibainisha kuwa wao wana nafasi kubwa zaidi ya kuona kinachoendelea kwenye jamii na akatoa wito kwao kuhakikisha wanafikisha huduma kwenye maeneo ya vijijini.
Musa Sang'anya, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali amefafanua kuwa jukwaa hilo lilizinduliwa na Rais Samia na kwamba ni mwaka wa pili mfululizo linafanyika na mwezi Oktoba Makamu wa Rais atakua Mgeni Rasmi kwenye kilele kitakachofanyika jijini Dodoma kitaifa.
Katibu Mkuu Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Serikali Revocatus Sono ameyataka mashirika hayo kufuata sheria na kanuni kama zinavyoelekezwa na sheria namba 24 ya mashirika yasiyo ya Serikali ya mwaka 2002.
Janeth Shishila Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza ambaye ni Msajili msaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoa wa Mwanza ametumia wasaa huo kuzitaka asasi hizo kutoa taarifa ya shughuli wanazofanya mkoani humo ili serikali iweze kutambua mchango wao mkoani humo.
Jukwaa hilo la siku mbili Mkoa wa Mwanza limechagizwa na Kaulimbiu isemayo Mashirika Yetu, Maadili yetu, Taifa Letu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.